WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF) na amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuuchunguza mwenendo wake tangu ulipoanza.

Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wadau wa zao hilo katika kikao cha kujadili maendeleo ya zao la kahawa mjini Dodoma. Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini mfuko huu haukuanzishwa kisheria bali wadau wake walishirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).
“Wakati Serikali inapambana kupunguza makato ya ovyo kwa wakulima, kumbe huku kuna chombo cha kuwachukulia fedha wakulima hii haikubaliki,” alisema Majaliwa. Aliagiza kufungwa kwa ofisi za CDTF kupisha uchunguzi na CAG akikamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti, kazi zilizokuwa zinafanywa na mfuko huo sasa zitafanywa na Bodi ya Kahawa.
Alisema majukumu ya kuundwa kwa CDTF yanaingiliana na ya Bodi ya Kahawa ambayo ni kufuatilia maendeleo ya zao hilo hivyo hakuna haja ya vyombo viwili vinavyofanya kazi moja.
Waziri Mkuu alipiga marufuku wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wanavijiji badala yake kahawa yote itauzwa kwa njia ya minada. “Kahawa itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali kwa watu kununua kahawa kwa wananchi vijijini marufuku kuanzia sasa.
Kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi,” alisema Waziri Mkuu. Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia uuzwaji wa zao hilo na kuwachukulia hatua wote watakaokutwa wananunua kahawa kwa wakulima.
“Anayetaka kahawa akanunue mnadani na si kwa wanavijiji lengo ni kuhakikisha mkulima anapata tija.” Waziri Mkuu alizidi kuonya. Pia aliziagiza halmashauri zote zinazolima kahawa nchini kuanzisha vitalu vya miche ya kahawa na kuigawa bure kwa wakulima.
Waziri Mkuu, Majaliwa pia aligiza maofisa Kilimo kuwaelimisha wakulima wote wenye miti mikongwe kuanzisha mashamba mapya. Kuhusu utafiti wa zao hilo, aliiagiza Wizara ya Kilimo itumie vyuo vyake vya kilimo kuanzisha vituo vya utafiti vitakavyofanya kazi hiyo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Joseph Kakunda alisema watahakikisha maagizo hayo yanafanyiwa kazi ambapo aliwaagiza wakuu wa mikoa yote 16 inayolima kahawa na wakuu wa wilaya wake 52 kufuta vibali vya ununuzi wa kahawa katika vyanzo vya mapato.
Kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Hazina, Dodoma kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Dk Chales Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Tamisemi, Kakunda.