MFANYABIASHARA Boniface Mbilinyi (32) mkazi wa Tabata Segerea, Dar es Salaam anashikiliwa na Polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kusafi risha Dola za Marekani 123,000 Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Anadaiwa kusafiri na kiasi kikubwa cha fedha ambapo dola za Marekani 83,000 hazikutolewa taarifa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jambo ambalo ni kosa na ni kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Matanga Mbushi alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo juzi 9:30 alasiri uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) eneo la juu la kuondokea abiria Terminal II.
Alisema maofisa wa usalama walimkamata abiria huyo Mtanzania mwenye hati ya kusafiria namba AB 757247 aliyekuwa amekata tiketi ya Shirika la ndege la Emirates akienda Dubai.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa akisafirisha dola za Marekani 123,000 ambapo alitoa taarifa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya dola 40,000 tu ambayo ni pungufu ya dola 83,000 ambazo hazikutolewa taarifa,” alisema.
Alisema abiria huyo alikuwa akienda Dubai kwa safari ya kibiashara na kiasi cha fedha ambazo hazikutolewa taarifa, hivyo wamezizuia na kuziweka akaunti ya dola ya Kitengo cha Kiintelijensia cha Fedha (FIU) namba 20110028135.
Alisema kwa sasa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi Terminal One JNIA kwa mahojiano zaidi na jalada lake litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua zaidi za sheria leo. Kamanda Mbushi alisema Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa fedha haramu inaelekeza mtu anapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha na anahitaji kukisafirisha ni lazima atoe taarifa.