WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amewataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanahifadhi vyema mapato ya fedha na kuyaweka wazi kwa waumini ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima kwenye nyumba za ibada.

Aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Shinyanga kwenye ibada ya kumuweka wakfu na kitini askofu wa pili wa dayosisi hiyo Johnson Chinyong’ole ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Angilikana nchini kisha mwaka jana kupendekezwa kuwa askofu.
Kabudi aliwataka viongozi wa dini kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanahifadhi vizuri mapato ya fedha kwa kuhakikisha yanaonekana kwa waumini ili kuondokana na migogoro inayoibuliwa ndani ya nyumba za ibada ikihusishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.
“Tunatambua Kanisa la Angilikana limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za kijamii kama maji, elimu na afya pale ambapo serikali imekwama kupafikia. Dayosisi hii ni yenu wala siyo ya wazungu hivyo ni wajibu kwenu kuhakikisha mapato ya fedha anaonekana ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima kati ya viongozi na waumini,” alisema Waziri Kabudi.
Aliongeza: “Serikali haina dini lakini ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa na dini yake hivyo viongozi wa dini wanatakiwa kuwa kiungo kati ya waumini na askofu ikiwa kuwakumbusha kupiga vita rushwa, vitendo vya kishirikina na ufisadi ambao serikali ya Rais Dk John Magufuli imekuwa ikipiga vita kila siku”.
Pia alitoa rai kwa askofu aliyewekwa wakfu na kitini, Chinyong’ole kuwa awakumbushe waumini maadili ya kanisa katika kuwajenga kiroho na kiuchumi lakini pia kutumia uongozi wake kuwajenga waamini ili waweze kushirikiana kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ambaye ni mlezi wa kanisa hilo alisema kuwa kanisa hilo limepitia wakati mgumu kwani kulikuwa na vuguvugu la migogoro kwa baadhi ya waumini kujidai wanazishika nyadhifa ambazo kuzipata zimeonekana kumbe kunautaratibu wake hivyo kushikamana na kwa umoja na kuepuka migogoro.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Jacob Chimeledya alisema kuwa kuna kazi kubwa na kwamba hali iliyopo ni mapito hivyo aliiomba serikali kulisimamia kanisa hilo kiuchumi kwani tayari limeanza mchakato wa kuanzisha chombo chake cha kusimamia na kuliangalia mali zake.