Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema mtangulizi wake Robert Mugabe alikuwa amesahau kwamba alikuwa amemfuta kazi kama makamu wake.
Amesema waliwasiliana wakati wa mzozo ambao hatimaye ulipelekea kuondolewa kwake madarakani.
Rais Mnangagwa amesema waliwasiliana kwa simu na kiongozi huyo wa miaka 93 ambaye alimwuliza ni kwa nini alikuwa nje ya nchi.
Aliigiza sauti ya Mugabe: "Emmerson. Uko wapi? 'Afrika Kusini. Unafanya nini huko? 'Ulinifuta kazi...ulinifuta kazi wiki iliyopita."
Bw Mnangagwa aliyasema hayo Alhamisi wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja nchini Msumbiji, tovuti ya New Zimbabwe imeripoti.
Bw Mnangagwa amesema baadaye Bw Mugabe alimhimiza kurejea Zimbabwe, lakini alimjibu kuwa "kuna watu wanaoukuzunguka ambao wanataka kuniangamiza."
Alisema kwamba anahofia maisha yake.
Bw Mnangagwa alikuwa anahusika katika kampeni ya kujaribu kumzuia mke wa Mugabe, Grace, kumrithi kiongozi huyo mkongwe.
Alifutwa kazi na kuondoka nchini humo.
Jeshi lilichukua udhibiti wa serikali na mwishowe kumuondoa madarakani Mugabe aliyekuwa ameongoza nchi hiyo kwa miaka 37.
Bw Mnangagwa alirejea nchini humo na akaapishwa kuwa rais mnamo 24 Novemba.
|
0 Comments