Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza jambo wakati wa mkutano na wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Mkoani Mtwara, Leo 19 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Wachimbaji wa madini ya Jasi na
Chumvi Mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa Mkutano wa pamoja na wachimbaji hao kwenye ofisi za Madini Kanda ya kusini, Leo 19 Januari 2018.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Kanda ya kusini Ndg Peter Ludovick akieleza kero za wachimbaji mbele ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo, Leo 19 Januyari 2018.

Na Mathias Canal, Mtwara

Wizara ya Madini imesisitiza wachimbaji wadogo na
wakubwa nchini kutambua umuhimu wa ulipaji kodi kwa kila wanachozalisha kwani
itasaidia kuongeza pato la Taifa kwa kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili nchi ikiwemo ukarabati wa miundombinu, Ujenzi na uimarishaji Wa
sekta ya afya, elimu, Sekta ya umeme na sekta ya maji.

Akizungumza Mkoani Mtwara wakati wa mkutano na
wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka
Biteko amesema kuwa jamii bado haina elimu ya kutosha juu ya ulipaji kodi hivyo
ofisi za madini nchini zinapaswa kuongeza msukumo Wa utoaji elimu juu ya
ulipaji kodi na utunzaji wa kumbukumbuku za shughuli za uvunaji Madini kwa kila
mahali kwenye leseni.

Mhe Biteko alisema kuwa wachimbaji wadogo kote nchini
wanapaswa kutambua kuwa hawatakiwi kusalia kukwepa kodi badala yake wanapaswa
kutoka kwenye uchuuzi na hatimaye kuhamia kwenye ufanyabiashara na kuhifadhi
taarifa zote kwa mujibu wa kanuni kwa kipindi cha miaka 5.

Alisema kuwa mtu yeyote anapoitwa mfanyabiashara
anatambulika katika jamii na serikali kwa ujumla wake hivyo kigezo kikubwa na
muhimu kwa mfanyabiashara ni kulipa kodi kwa mujibu Wa kanuni, sheria na
taratibu.

Akizungumza kwa msisitizo Mhe Biteko alisema kuwa
watanzania wamempata Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuongoza Taifa akiwa Rais Wa
Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano hivyo wanapaswa
kuunga mkono juhudi za utendaji wake kwa kulipa kodi kwa manufaa ya jamii
nzima.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Wa Madini
ameupongeza uongozi Wa Ofisi ya Madini Kanda ya Mtwara kwa ushirikiano mzuri na
wachimbaji jambo ambalo limeimarisha utendaji wao pasina malalamiko dhidi ya
serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti Wa Chama Cha wachimbaji
Mkoa Wa Mtwara Ndg Festo Balegele akizungumza wakati Wa mkutano huo alimsihi
Naibu Waziri wa Madini kutilia mkazo uongezaji thamani wa chumvi inayozalishwa
nchini kwa kuikausha (Drying) na kuisaga (Grinding) sambamba na kuongeza Madini
joto kwani itapelekea serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumiwa na
serikali kuagiza chumvi nje ya nchi.

Alisema kuwa kila mwaka jumla ya tani 350 za chumvi
huagizwa nje ya nchi ambapo ikiwasili nchini inauzwa kwa shilingi 500 kwa gramu
500 sawa na shilingi 50,000 kwa kilo 50 kiasi ambacho ni kikubwa Mara tano ya
gharama za chumvi inayozalishwa nchini kwani inauzwa kwa shilingi 5000 kwa kilo
50.

Alisema kuwa chumvi inayoagizwa nje ya nchi ni kiasi
cha Tani 350,000 kila mwaka huku akisisitiza kuwa serikali ingetilia mkazo na
kuboresha miundombinu nchini ingerahisisha upatikanaji wa chumvi nyingi nchini
ambayo inauzwa kwa kiasi kidogo chenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya watanzania.

MWISHO