|
KUANZA kwa safari za Meli za kisasa za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma ambazo zina uwezo wa kubeba uzito wa tani 1,000 kumefungua fursa za kibiashara kati ya Tanzania, Malawi na Msumbiji.
Meli ya Mv Njombe ambayo imefanya safari yake kwa mara ya kwanza nchini Malawi imefika salama na kutia nanga katika bandari za Nkhata Bay. Meli ya Mv Ruvuma inayopakia shehena ya Cnilnker inatarajiwa kutia nanga katika Bandari ya Monkey Bay nchini Malawi siku mbili zijazo.
MV Njombe ambayo ilibeba takribani tani 800 ya shehena ya saruji kutoka bandari ya Kiwira nchini Tanzania hadi bandari ya Nkhata Bay nchini Malawi imetia nanga salama na imetumia muda mfupi zaidi kufika Malawi.
MV Ruvuma ambayo ni pacha wa MV Njombe nayo imepakia takribani tani 800 za shehena ya ‘Clinker’ katika bandari ya Kiwira nchini Tanzania kuelekea bandari ya Monkey bay nchini Malawi.
Akizungumzia ujio wa shehena hizo za Saruji na ‘Clinker’, Balozi wa Tanzania nchini Malawi ambaye pia alikuja kushuhudia tukio hilo, Mheshimiwa Benedicto Mashiba amesema kwamba kuanza kwa safari hizo ni habari njema kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Malawi .
Balozi Mashiba amesema kwamba, ujio wa meli hizo ni ufunguo wa biashara kati ya Tanzania na Malawi kwani kusafirisha bidhaa kwa njia ya maji ni nafuu na salama zaidi ukilinganisha na barabara.
“Usafiri huu ni mkombozi kwa wananchi na wafanyabiashara wa nchi hizi mbili (Malawi na Tanzania) kwani utawezesha usafirishaji wa mizigo kwa wingi ukilinganisha na njia nyingine kama barabara,” amesema Balozi Mashiba.
Mashiba amesema kwamba kuna biashara kubwa ya kusafirisha mizigo kati ya Tanzania, Malawi na Msumbiji kupitia Ziwa Nyasa hivyo kuanza safari kwa meli hizo kutasaidia kuongeza zaidi ukubwa wa shehena katika ya nchi hizo.
Naye Mkuu wa bandari za Ziwa Nyasa, Ajuaye Msese amewasihi wananchi na wafanyabiashara wa Tanzania, Malawi na Msumbiji kutumia usafiri huo kwani ni wa uhakika, nafuu na salama.
Msese amesema kwamba kusafirisha shehena ya bidhaa kama ‘Clinker’, saruji na makaa ya mawe pamoja na bidhaa nyingine kwa wingi ni salama zaidi ukitumia njia ya maji kuliko barabara.
Amesema mbali na hilo na usalama na unafuu, lakini pia tukisafirisha bidhaa kwa kutumia maji tunaokoa uharibifu wa miundombinu yetu kama barabara na madaraja. Mkuu huyo wa bandari za Ziwa Nyasa alitolea mfano mzigo wa saruji ulioletwa na meli ya MV Njombe pekee, kama ungekuja kwa njia ya barabara, basi msafirishaji angelazimika kutumia malori 25.
“Ukisafirisha mzigo kwa njia ya maji ni nafuu, salama na unakuwezesha kusafirisha mzigo mkubwa zaidi kwa wakati mmoja,” amesema Msese. Kwa mujibu wa Bw. Msese, ukisafirisha mzigo kwa njia ya maji na kwa wingi kama huu, itamsaidia mlaji wa mwisho kuja kupata bidhaa hizo kwa bei nafuu.
Ziwa Nyasa ni moja kati ya maziwa makuu yanayounganisha mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Songea na nchi za Malawi na Msumbiji kwa njia ya maji.
0 Comments