JESHI la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia mtu anayejiita Nabii Tito Machibya (44) kwa kutangaza imani ya kidini inayokiuka maadili ya nchi na kuanzia sasa litawakamata watu watakaomshabikia na kuambatana naye.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Giles Muroto alisema uchunguzi wa awali umeonesha mtuhumiwa huyo ana ugonjwa wa akili wa muda mrefu.

Akielezea kukamatwa kwake alisema Januari 16, mwaka huu, mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa kosa la kueneza chuki ya kidini dhidi ya watu wengine kinyume na kifungu cha sheria namba 129 cha kanuni ya adhabu Sura ya 16 na marekebisho yake ya 2002.
“Anavaa majoho anatembea kwenye sehemu za starehe, anavaa msalaba kudhalilisha madhehebu ya dini ya Kikristo, anasambaza vipeperushi na CD zinazodhalilisha na kusema kunywa pombe si dhambi, kuzaa na house girl sio dhambi, anatumia Biblia kutoa tafsiri potofu,” alisema.
“Mtuhumiwa huyu amekamatwa baada ya kurekodi vipande vifupi vya matangazo ya video na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini nyingine na kuleta chuki na kurusha kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.
Pia alisema mtuhumiwa huyo amekuwa akisambaza vipeperushi mbalimbali katika maeneo ya starehe akitangaza imani ya dini inayokiuka maadili ya nchi na kufanya hadharani vitendo visivyofaa akitumia kitabu cha Biblia ambacho pia hafungamani.
“Anatoa tafsiri za Biblia zenye upotoshaji, kufanya vitendo vya udhalilishaji hadharani na kuchochea maovu katika jamii, akishirikiana na wanawake wawili anaodai kuwa ni wake zake mmoja wao akiwa kijakazi wake (house girl).
Kamanda Muroto alisema uchunguzi wa awali unaonesha Juni 23, 2014 alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutibiwa magonjwa ya akili na aliruhusiwa kutoka wodini na daktari wake Dk William na kutakiwa kurejea tena kwa uangalizi na tiba Julai 9, 2014 lakini hakurejea.
Aidha Kamanda Muroto alisema Januari 17, mwaka huu alifikishwa tena katika Hospitali ya Mirembe Dodoma kwa uchunguzi uliofanywa na Dk Dickson Phillip na kugundulika kuwa ni mgonjwa wa akili wa muda mrefu.
“Hali akiwa na ugonjwa huo wa akili lakini ameendelea kuhamasisha maovu yaliyo kinyume na maadili mema ya dini zote na desturi za watanzania huku akionekana ni mtu mwenye akili timamu na kupata watu watu wanaomshabikia na kuambatana naye,” alisema.
Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na majoho yenye misalaba miwili, vipeperushi 80, Biblia moja na msalaba, vifaa anavyotumia kutangaza imani inayokwenda kinyume na maadili mema ya taifa.
Alisema polisi inamshikilia ili kufanya uchunguzi wa kina dhidi yake, lakini pia kumnusuru yeye mwenyewe asiweze kudhuriwa na watu kwa kuwa anajenga machukizo dhidi ya dini na watu wengine wenye imani tofauti. Aidha Kamanda Muroto alisema kuwa nabii huyo hayupo kihalali na kwamba chini ya usajili wa taasisi za kidini sura ya 337 hayupo na hajasajiliwa.