Hugh Masekela, mwanamuziki maarufu wa mtindo wa jazz kutoka Afrika Kusini aliyechangia juhudi za kukabiliana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo, amefariki dunia akiwa na miaka 78.

Familia ya mwanamuziki huyo mcheza tarumbeta, kupitia taarifa, imesema Masekela amefariki akiwa mjini Johannesburg baada ya kuugua saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.
Masekela alipata umaarufu mkubwa kutokana na mtindo wake wa kipekee wa Afro-Jazz na vibao vilivyokuwa maarufu kama vile Soweto Blues.
Wimbo huo alioutoa 1977 ulihusika sana katika harakati za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.
Amekuwa akitambuliwa na wengi kama "baba wa Jazz nchini Afrika Kusini.
Alizaliwa mnamo Aprili tarehe 4 1939. Anasifika kwa ujuzi wake kupuliza tarumbeta na alikuwa ni mojawapo ya wakosoaji wa wazi wa ubaguzi wa rangi.

Jitihada za Masekela dhidi ya ubaguzi wa rangi

Nyimbo zake zililenga jitihada za kupigania uhuru.
Alizaliwa katika mtaa uliopo kaskazini mashriki, alianza kuimba na kupiga kinanda akiwa mtoto.
Akiwa na umri wa miaka 14 alianza kupiga tarumbeta baada ya kutizama filamu ya hollywood kumhusu mwanamuziki wa Kimarekani mwa mtindo wa Jazz.
Alikabidhiwa tarumbeta yake ya kwanza na Trevor Huddleston, aliyekuwa askofu baadaye aliye kampeni dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Masekela na baadhi ya wanafunzi wenzake shuleni waliunda bendi iliyojulikana kama Huddleston Jazz Band, bendi ya kwanza ya Okestra ya vijana Afrika kusini.
Mwishoni mwa miaka ya 1950 alikwenda Marekani na kuunda urafiki na Harry Belafonte na akajiunga na shule ya muziki.
Hugh Masekela with Femi KutiHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionAlisaidia kutumbuiza wakati wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia 2010 Afrika Kusini na mwanamuziki mwenzake Femi Kuti
Unyanyasaji ulioshuhudiwa Afrika kusini ulimpa shinikizo katika kutunga muziki wake na harakati zake za kisiasa.
Muziki wale ulidhihirisha jitihada, huzuni, furaha na ari ya wananchi wa Afrika kusini.
Kufuatia mauaji ya kimbari huko Sharpeville mnamo 1961, Masekela alikwenda uhamishoni nchini Marekani.
Alimuoa muimbaji Miriam Makeba licha ya kwamba walitalikiana miaka miwili baadaye.
Wimbo wake uliovuma mnamo 1987 "Bring Him Back Home" ulikuwa wimbo mkuu uliokuwa unachezwa katika kila ziara ya Nelson Mandela kote duniani baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.
Katika wasifu wake, Masekela alielezea jitihada zake dhidi ya ubaguzi wa rangi na jitihada zake binafasi za kupambana na uraibu wa pombe.
Atakumbukwa kuwa mojawapo ya watu wenye sauti kubwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi na Afrika kusini mpya iliyofuata baadaye.