Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kusitisha misaada kwa taifa la Palestina iwapo litakataa kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Wizara ya maswala ya kigeni imethibitisha kuwa alikuwa akizungumzia msaada wa kiuchumi na usaidizi wa kiusalama.

Bwana Trump aliishutumu Palestina kwa kuivunjia heshima Marekani akisema ''kwa nini tuwafanyie kitu na wao wenyewe hawatufanyii chochote''.
Palestina imeikataa Marekani kuwa mpatanishi asiyependelea upande wowote katika mazungumzo hayo ya amani.
Wamekasirishwa na hatua ya Washington kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Afisa aliyekuwa akiongoza ujumbe wa mazungumzo upande wa Palestina Saeb Erakat alijibu matamshi ya hivi karibuni ya rais Trump: Trump anaweza kununua vitu vingi na fedha lakini hawezi kununua heshima yetu.
Akizungumza katika kongamano la kiuchumi mjini Davos, Switzerland, bwana Trump alisema kuwa Marekani inawapatia Palestina mamia ya mamilioni ya madola kama msaada na usaidizi kila mwaka.
Alilalamikia hatua ya uongozi wa Palestina wa kukataa kukutana na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence katika eneo hilo mapema wiki hii.
Amesema kuwa yeye ndio rais wa kwanza kwa kuhusisha msaada na mpango wa amani.
''Hizo pesa ziko katika meza lakini hazitawafikia hadi pale watakapokubali kuketi katika meza ya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu''.
''Ninaweza kuthibitisha kwamba Israel inataka kuanza mazungumzo ya amani nao, na wao Palestina watalazimika kukubali kuanza mchakato huo ama la sivyo hatutashughulika tena''.