Wazazi wawili wamekamatwa huko California baada ya polisi kupata watu 13 waliokuwa wameshikiliwa mateka nyumbani kwao wakiwemo wengine waliofungiwa kwenye vitanda vyao kwa minyororo na makufuli.
David Allen Turpin, 57, na Louise Anna Turpin, 49, walikamatwa kwa tuhuma za mateso na kuhatarisha maisha ya watoto.
Watu hao 13 walio na umri wa kati ya miaka miwili na 29, walipatikana kwenye nyumba eneo la Perris kilomita 95 kusini mashariki mwa Los Angeles.
Maafisa waligundua hilo siku ya Jumapili wakati mmoja wa watoto hao alifanikiwa kuponyokana na kupiga namba ya dharura akitumia simu ambayo alipata ndani ya nyumba.
Msichana huyo ambaye polisi wanasema alionekana kuwa na umri wa miaka 10, alidai kuwa ndugu zake wengine 12 walikuwa wakishikiliwa na wazazi wao.
Polisi baadaye walipata watoto kadhaa wakiwa wamefungiwa kwenye vitanda vyao kwa nyororo na makufuli gizani katika mazingira yenye harufu mbaya.
Lakini wazazi hawakuweza kutoa sababu ni kwa nini watoto hao walifungwa kwa njia kama hiyo.
Polisi walishangazwa kugundua kuwa saba kati ya wale waliokuwa wakizuiliwa kwenye nyumba hiyo walikuwa ni watu wazima wa kati ya umri wa miaka 18 na 29.
Waathirirwa walioneka kudhoofika kiafya na wachafu.
Waathiriwa hao wote kwa sasa wanatibiwa kwenye hospitali za eneo hilo.
Tunafahamu nini kuhusu familia hiyo?
Kulingana na rekodi, wazazi hao waliishi Texas kwa miaka mingi kabla ya kuhamia California.
Bw Turbin anatajwa kuwa alikuwa na kazi nzuri kama mhandisi kwenye kampuni ya ndege na teknolojia ya ulinzi ya Northrop Grumman.
Hata hivyo kutokana na kuwa na watoto wengi na mke wake kutokuwa na kazi, matumizi yake yalizidi kipato chake na mara mbili alitangazwa kufilisika.
Kwenye tovuti ya elimu ya California Bw Turpin anatajwa kuwa mkuu wa shule ya Sandcastle, ambayo ni shule ya kibinafsi iliyo nje ya nyumba yake.
Shule hiyo ilifunguliwa mwezi Machi mwaka 2011, kwa mujibu wa mtandao huo. Watoto sita walijiunga na shule hiyo katika viwango tofauti.
Wazazi wake Bw Turpin walisema kuwa wajukuu wao walisomea nyumbani lakini hawajaiona familia hiyo kwa miaka minne au mitano.
0 Comments