Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira asitishe uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).

Alitoa agizo hilo juzi jioni wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Serengeti, wilayani Tarime, Mara. Alichukua hatua hiyo baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza sharti la mtaji la Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
KCBL inatakiwa kutimiza sharti la kuwa na mtaji kamili wa Sh bilioni tano katika kipindi cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo. Majaliwa alisema ni marufuku kuuza mali za ushirika huo, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali vya ushirika nchini.
Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali za vyama vya ushirika na watakaobainika kuhusika na ubadhirifu watachukuliwa hatua. Januari 4, 2018, BoT ilizipa miezi sita, benki tatu nchini ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji wake unaohitajika kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa kutosha.
Benki hizo ni Kilimanjaro Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Bank Plc na Tandahimba Community Bank Limited, zikishindwa kutekeleza zitachukuliwa hatua. BoT itazifutia leseni na kusimamisha shughuli zake chini ya ufilisi benki hizo zikishindwa kutekeleza agizo hilo kufikia Juni 30, 2018.