MTAALAMU bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Koheleth Winani, amesema ni uzushi kusema makutano ya kimwili baina ya baba na mjamzito, humwathiri mtoto tumboni.

Dk Winani ambaye pia ni Mratibu wa Uzazi Salama katika wizara hiyo, alisema hayo hivi karibuni alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa sio kweli kwamba mapenzi wakati wa ujauzito, humwathiri na kumchafua mtoto.
Akizungumzia hatari zinazomkabili mwanamke mwenye mimba ya pacha wengi, alisema ni uwezekano wa watoto kukaa vibaya tumboni na wengine kuzaliwa wakiwa wameungana, au kuwa na ulemavu.
Alisema, "mimba inapokuwa katika hali ya kawaida, wanandoa waendelee kuhusiana hadi mjamzito atakapofikia hatua ya kushindwa, lakini wazingatie kuwa mjamzito asilalie tumbo na hali hiyo, inaongeza upendo baina yao."
Kuhusu pacha kuungana, alisema: "Uwezekano wa watoto kuungana unaweza kutokana na yai kuwa na mbegu moja ambayo mgawanyiko wake haukamiliki."
Mtaalamu huyo aliwahimiza wajawazito kuhudhuria kliniki na kwamba siku ya kujifungua inapowadia, waliobainika kuwa na mimba za pacha waende hospitali.
"Wajawazito wapate mlo kamili, muda wa kupumzika na kuzingatia kufanya mazoezi madogo ya kawaida na sio kulala tu hadi kutaka kuoshwa," alisema Dk Winani.