BENKI ya TPB imeungana na taasisi ya Savings at the Frontier (SatF) katika mradi wa dola za Marekani milioni moja wa kuunganisha wateja na mfumo rasmi wa fedha.
Mradi huo Digitalizing Informal Savings Mechanisms utaendeshwa kwa miaka mitatu na TPB itawaunganisha mfumo rasmi wa fedha wateja wapya 250,000 ifikapo mwaka 2020. Hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi kwa waandishi wa habari Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Alisema mradi huo utaanzia mkoa wa Ruvuma, na kupelekwa Mtwara, Lindi, Njombe, Iringa na Morogoro kuboresha huduma za kifedha.
“Watanzania wengi waishio mikoa ya pembezoni hususani wenye vipato vidogo wana changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma za kifedha. Kupitia ushirikiano huu na SatF, TPB itawawezesha wananchi kupitia makundi au mtu mmoja mmoja, kujiwekea akiba kwa teknolojia rahisi na salama isiyowalazimu kwenda kwenye tawi la benki ili kupata huduma hizo za kifedha.
“Njia hii itawawezesha wananchi kutatua changamoto zao za kifedha na pia kuwaingiza kwenye mfumo rasmi wa kiuchumi,” alisema.
Alisema TPB ni benki ya kwanza kuanzisha utoaji wa huduma za kibenki kwa makundi kupitia simu za mkononi, TPB POPOTE. ‘Hivi sasa, wateja kupitia vikundi vyao wanaweza kuweka akiba na hata kukopa kupitia simu zao za mkononi,” alisema Moshingi.
Meneja wa mradi kutoka programu ya SatF, Steve Peachey alisema benki ya TPB ndio ya kwanza kufanya kazi na taasisi yake hapa nchini, na walivutiwa na namna ambavyo TPB imeonesha dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi hao kupata huduma za kifedha.
Pia alisema taasisi yake inafurahia kupata nafasi ya kufanya kazi na TPB, taasisi ya fedha yenye sifa na historia ndefu katika kupeleka huduma za kifedha kwa wananchi wake popote walipo. Hii ni fursa nzuri kwa SatF na TPB kujenga umoja imara kuwafikia wananchi maskini.
“SatF ni programu maalumu yenye malengo ya kuhakikisha huduma za kifedha za uhakika zinawafikia wananchi wengi walio nje ya mifumo rasmi ya kibenki, programu hii inaratibiwa na shirika la Oxford Policy Management kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya MasterCard Foundation, madhumuni yakiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na jamii zenye vipato vya chini kwenye nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara,” alifafanua Peachey.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Finscope mwaka 2017, asilimia 59 ya Watanzania wana vipato vya msimu na kati ya changamoto zinazowakabili kubwa ni uwezo wa kumudu gharama za matibabu, ada za shule.
Utafiti huo pia ulionesha asilimia 40 ya Watanzania hukopa fedha kutoka kwa jamaa ama rafiki kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za kifedha zinapojitokeza kwao.
Watanzania milioni 7.8 hawapati huduma za kifedha na hili limeleta uhitaji mkubwa wa mazingira bora ya kuwawezesha wananchi hao kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba ili kukabiliana na changamoto za kimaisha.