RAIS John Magufuli amewasili salama jijini Kampala kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Rais Magufuli aliondoka leo asubuhi jijini Dar es Salaam, na tayari amekutana na mwenyeji wake, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni Ikulu ya Entebbe.

Magufuli yupo Uganda na viongozi mbalimbali wa Tanzania akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga.
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko amesema, mkutano wa siku mbili wa wakuu wa nchi EAC unatarajiwa kujadili masuala ya miundombinu ndani ya nchi sita za EAC, afya na maendeleo kwa ujumla.
Nchi wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya EAC kwa umma, mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wajumbe zaidi ya 1,000 wa ndani na nje ya nchi wanachama wa jumuiya.
Wakuu wa nchi wanatarajiwa kujadili masuala ya miundombinu, fedha za tiba na maendeleo kwa kutumia kaulimbiu ‘Kukuza na kapanua mtangamano kwenye miundombinu na maendeleo ya sekta ya afya kwenye nchi wanachama EAC’.
Mkutano wa Kampala umeandaliwa na sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na nchi wanachama wa jumuiya hiyo, na wadau wakubwa wa maendeleo kwenye eneo hilo.
Utakuwa mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi za EAC kuzungumzia masuala ya afya na utakuwa wa nne kuhusu kugharamia miundombinu na maendeleo.
Mkuu wa Mawasiliano kwenye Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno kupitia taarifa yake amesema wakuu wa nchi wanatarajiwa kuzungumzia maendeleo ya miradi ikiwemo miundombinu bora, ya uhakika, endelevu, imara na inayotolewa haraka ikiwemo wa kieneo na ile ya kuvuka mipaka ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi na hali bora za mwananchi.