CHUO Kikuu cha Makerere nchini Uganda kimewasimamisha masomo wanafunzi 17 waliofanya udanganyifu na kugushi ruhusa ya kufanya mitihani katika mwaka wa masomo 2017/2018.
Wanafunzi hao wanasoma kwa utaratibu wa kusoma bila kuwepo chuoni hapo na kwa muda wote (SODLL).
Kwa mujibu wa taarifa ya msajili wa chuo hicho, Tom Otim, baadhi ya wanafunzi wamesimamishwa moja kwa moja na wengine wamesimamishwa kwa miaka miwili, na mmoja kwa mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa Otim, kamati ya SODLL ya masuala ya makosa na ukiukwaji taratibu za mitihani ilikaa na kutoa uamuzi huo na kwamba, wanafunzi waliosimamishwa walihusika kwenye udanganyifu wa aina mbalimbali kwenye mitihani.
Taarifa ya Otim imewataja wanafunzi waliosimamishwa moja kwa moja kuwa ni Alex Kintu, Elvis Ounde, Winifred Nnakyeyune na Ruth Kayaga.
Wanafunzi hao waligushi ruhusa ya kufanya mitihani. Wanafunzi waliosimamishwa kwa miaka miwili ya masomo ni Martha Atuheire, Lawrence Kiwika, Sharon Namanya, Angela Awori na Grace Kiyemba.
Wanafunzi hao waligushi ruhusa ya kufanya mitihani. Wanafunzi watatu wameonywa na matokeo yao yamefutwa kwa kuwa walifanya udanganyifu kwenye mitihani.
Wanafunzi hao ni Hope Katushabe, Ciccy Kanyiginga na Anna Mirembe.
Wanafunzi wanned wamesimamishwa kwa mwaka mmoja wa masomo kutokana na udanganyifu kwenye mitihani.
Taarifa ya Otim imewataja kuwa ni Swabrah Nkyazze, Stella Biraalo, Racheal Lilian Kanyesigye na Shiforah Prishaba. Mwanafunzi Dickson Oscar, amesimamishwa moja kwa moja kwa udanganyifu kwenye mitihani.
|
0 Comments