MAOFISA ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wamepewa wiki tano hadi Machi 31, mwaka huu, kuhakikisha wanapima mashamba na viwanja katika eneo la Ndachi Kata ya Mnadani ili kumaliza mgogoro, uliodumu kwa muda mrefu baina ya wenyeji na wageni.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ametoa muda huo kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika shambani hapo baada ya kupokea ripoti ya tume yaliyoiunda kuchunguza mgogoro na kutafuta suluhu, baada ya kudumu kwa muda mrefu na kusababisha ugomvi baina ya wenyeji na wahamiaji.
Dk Mahenge alisema amepitia mapendekezo na kujiridhisha kwamba mgogoro huo upo baina ya wenyeji na watu waliohamia au kuingia katika eneo hilo, lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 5,300 na viwanja zaidi ya 1,500.
Amemwagiza Katibu Tawala pamoja na maofisa ardhi kutoka halmashauri za wilaya nyingine kwa kushirikiana na wa Manispaa, kupima viwanja vyote katika eneo hilo, ambalo awali lilikuwa limetengwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA) kwa ajili ya kuendesha kilimo, lakini baadaye likageuzwa kuwa viwanja.
Pia alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, kuhakikisha hakuna shughuli za ujenzi, kuuziana viwanja au nyingine, katika muda huo na atakayebainika akikiuka amri hiyo, basi achukuliwe hatua.
Katika kuhakikisha wanapata uhakika wa eneo na wamiliki wa viwanja hivyo, Dk Mahenge alitaka Halmashauri ya Manispaa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo, kutambua miliki zote za viwanja hivyo, lakini pia kufuatilia kesi zote zilizopo mahakamani, zilizotolewa uamuzi na kujua utekelezaji wake ukoje.
Amewataka wananchi wa eneo hilo, kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa wapimaji, watakaoweka kambi katika eneo hilo, ili kubaini wamiliki halali wa eneo hilo, ambalo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu, iliyohatarisha amani kwa muda mrefu.
Ameitaka Halmashauri ya Manispaa kuandaa orodha kamili ya wananchi wenye viwanja na mashamba yenye nyaraka na yasiyo na nyaraka, yanayolipiwa na yasiyolipiwa na kupeleka orodha hiyo pamoja na mapendekezo ya matumizi ya mipango miji katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza kabla, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alisema, mgogoro huo una sura nyingi zikiwemo za wenyeji ambao walikuwapo miaka mingi na baadaye wakaja watu wengine na kuingia katika maeneo hayo kutokana na kwamba yalikuwa hayaendelezwi.
Amesema baadhi ya viwanja vina watu wawili wenye hatimiliki na wengine wana barua za toleo, baadhi yao wakimiliki mashamba na kati ya 1988 hadi 1990 kutoendeleza na wageni wakaamua kuanza kulima na baadaye wakaanza kujenga makazi bila kujua kama yana watu.
|
0 Comments