JESHI la Polisi mkoani Mwanza, kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) mkoani hapa, limemkamata Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Anthony Bahebe.

Pia Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Alphonce Sebukoto naye amekamatwa na Jeshi hilo. Viongozi wote hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu wa fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kukamatwa kwa viongozi hao, kunatokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.
Kamanda Msangi alisema, Sebukoto alikamatwa Februari 19, mwaka huu na Bahebe alikamatwa jana. Wote wanaendelea kuhojiwa na Polisi kwa kushirikiana na Takukuru.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale alisema Sebukoto aliidhinisha malipo ya Sh milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bahebe. Alisema Sebukoto aliidhinisha malipo hayo kwa Bahebe Novemba, mwaka jana wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi, ambapo jumla Sh milioni 138 ziliingizwa katika akaunti binafsi ya mwenyekiti huyo.
Alisema kiasi kingine cha fedha, kinachunguzwa kubaini kilipo. Kukamatwa kwa viongozi hao, kunatokana na juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.
Februari 19, mwaka huu akiwa katika ziara yake wilayani Misungwi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi Sebukoto na kuagiza achunguzwe na vyombo husika.
Alichukua hatua hiyo baada mwanasheria huyo, kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya Sh milioni 278.
Alisema mwanasheria huyo Novemba, mwaka jana alipokuwa anakaimu nafasi ya mkurugenzi, aliidhinisha malipo ya Sh milioni 278 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bahebe.
Waziri Mkuu alisema Bahebe aliishitaki halmashauri hiyo, akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge, uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.
Alisema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo, wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba, 2015.
Alisema mwanasheria alimlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na halmashauri, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma. Aliwakumbusha watumishi wa umma, kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.