Treni ya kubeba abiria iliyokuwa safarini kutoka Dodoma kwenda Kigoma kupitia Tabora imepata ajali katika eneo la kijiji cha Mpeta, wilayani Uvinza kaskazini magharibi mwa Tanzania, taarifa zinasema.
Watu watatu wamejeruhiwa

Ajali hiyo imesababishwa na kichwa cha treni kuacha njia na mabehewa mawili kuanguka, shirika la habari la kibinafsi la Azam limeripoti.
Kaimu meneja wa wamawasiliano wa Shirika la Reli la Tanzania (TRL) Mohamed Mapondela ameambia BBC kwamba watu watatu wamejeruhiwa.
"Sababu ya ajali bado haijafahamika lakini, timu ya kutathmini ajali iko njiani kuelekea eneo la tukio," amesema.
Ajali ilitokea majira ya saa saba na dakika hamsini mchana eneo la katikati ya stesheni ya Malagarasi na Uvinza.
"Tathmini kamili ya ajali itatolewa pale ambapo mabehewa yatakuwa yameinuliwa."

Kubaini chanzo cha ajali

Bw Mapondela amesema eneo hilo si kwamba ni baya na halina historia ya kupata ajali yoyote ile, ndio maana ni vigumu kusema nini hasa kinaweza kuwa chanzo cha ajali.
Mbunge wa Kigoma Zitto Kabwe ameandika kwenye Facebook kwamba amezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma na kufahamishwa kwamba chanzo cha ajali ni injini kupoteza njia kufuatia mchanga uliokuwa kwenye njia ya reli. "Naomba uchunguzi ufanyike ili kuona kama mchanga ule ni sababu ya mvua kubwa zinazonyesha ama la. Treni ndio usafiri wa wanyonge wengi mkoani kwetu hivyo ajali za namna hii zinastusha na kuogopesha. Natoa pole sana kwa wana Kigoma na Watanzania wengine," amesema.
Agosti mwaka jana watu watatu walifariki kwenye ajali iliyohusisha treni na gari la uchukuzi wa abiria mjini Morogoro.
Mmoja wa waliofariki alikuwa mwanafunzi aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 6. Wengine wawili walipoteza maisha wakati wakipelekwa hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na majeruhi wengine 29.