MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Geita imewaweka rumande maofisa wanne wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyarugusu mkoani Geita, kwa kupuuza amri halali ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Imedaiwa mahakamani kuwa maofisa hao walijenga na kutumia kienyeji miundombinu ya kuhifadhi topesumu, inayojulikana kitaalamu kama Tailings Storage Facility (TSF) katika Kijiji cha Ziwani wilayani Geita.
Mwanasheria wa Serikali, Anosisye Erasto amewataja washitakiwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Geita, Kaliho Mrisho kuwa ni Julius Malemi (41), Ludovick de Ferranti (27), Fredrick Masanja (51) na Alex Noni (31). Kesi yao itatajwa tena Machi 1, mwaka huu, siku maombi yao ya dhamana yatakaposikilizwa.
Wakili huyo wa serikali amedai kwamba washitakiwa kwa makusudi na kwa ukaidi, walitumia miundombinu ya TSF kienyeji katika kijiji cha Ziwani na kuhatarisha mazingira na maisha ya watu na viumbe wengine. Alidai kwamba wamefanya hivyo kinyume na Kanuni ya 40 na 176 ya Sheria ya Mazingira ya 2010.
Erasto amedai kwamba, washitakiwa siku hiyo ya Februari 23, mwaka huu katika kijiji hicho hicho, walitumia miundombinu hiyo bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kinyume na kanuni hizo mbili.
Amedai kuwa, washitakiwa wamekaidi amri halali ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Vedast Makota aliyoitoa Desemba 6, mwaka jana, kinyume na Kifungu cha 124 cha Kanuni ya Adhabu.
Erasto alidai kuwa washtakiwa, wametumia miundombinu hiyo bila cheti cha kutambua usalama wa mazingira kinyume na Kifungu cha 81 (1) (2) (3) (4) na 191 vya Sheria ya Kuhifadhi Mazingira 2004 na Kanuni 60 (1) na (2) (b) za Kuhami Mazingira za 2005.
Hakimu Mrisho aliamuru washtakiwa wawekwe rumande hadi Machi 1, mwaka huu siku kesi yao itakapotajwa kwa mara ya pili.
|
0 Comments