MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Seif Shekalaghe amesikitishwa na kitendo cha mwanafunzi wa kike wa darasa la nne katika shule ya msingi wilayani humo, kupewa ujauzito na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

Mwanafunzi huyo ni miongoni mwa wanafunzi 22 wa shule za msingi katika wilaya hiyo waliopata ujauzito kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 24 mwaka huu, huku wanafunzi 27 wa shule za sekondari wakiwa wamepata ujauzito kwa kipindi hicho.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Sekondari Shishiyu iliyopo wilayani humo wakati wa maandalizi ya kampeni aliyoianzisha ya kukomesha mimba shuleni yenye kauli mbiu isemayo,"Watoto wa Kike Wasome hadi Chuoni’’, amesema, ameshangazwa na kitendo cha mwanafunzi wa darasa la nne kupata ujauzito.
Amesema kuwa ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya watu wazima kujihusisha katika masuala ya kimapenzi na watoto wa kike wenye umri mdogo ambao bado wako shuleni, jambo ambalo halikubaliki katika jamii na hawezi kuvifumbia macho vitendo hivyo na kuamua kutumia nguvu zote kupambana nalo.
"Mimi binafsi nimeumizwa sana na jambo hili kwani huo ni ukatili kabisa yaani mtu mzima unakwenda kumrubuni mtoto mdogo na unafanya naye mapenzi hadi unampa ujauzito hii ni laana mie nimeamua kupambana na watu wote wanaofanya vitendo hivyo vya kuwapatia mimba wanafunzi," amesema kwa uchungu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Maswa, Paul Jidayi amesema, umefika wakati kwa wazazi kukaa na watoto wao na kuwakumbusha kuhusu madhara ya kuwepo kwa mimba za utotoni kwani serikali imeona umuhimu wa elimu na kuamua kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mkazi wa kijiji hicho, Solo Fumbuka, amesema wamekuwa wakikatishwa tamaa na jeshi la polisi katika wilaya hiyo katika mapambano hayo kutokana na jeshi hilo kuwaachia huru watuhumiwa wanaowakamata na kuwafikisha katika kituo kidogo cha polisi cha Shishiyu na kituo kikubwa cha polisi cha wilaya kilichopo mjini Maswa kutokana na makosa hayo.