MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu ya Pasaka inasherehekewa kwa amani na utulivu, na kwamba uhalifu wowote utakaojitokeza utadhibitiwa kwa haraka.
Ameyasema hayo kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, akiwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa jeshi hilo la Polisi. IGP Sirro alisema ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi umesaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa nchini.
“Kiujumla hali ya usalama hapa nchini ni shwari na matukio makubwa ya uhalifu wa kutumia silaha yamepungua kwa kiasi kikubwa na jitihada za kukabiliana na makosa ya usalama barabarani zinaendelea ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi kwa raia.
“Tunapoelekea kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote linawahakikishia wananchi kuwa limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu hii inasherehekewa kwa amani na utulivu na hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Kwa mujibu wa IGP Sirro, ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote wanasherehekea sikukuu hiyo katika hali ya utulivu.
“Wazazi wanatakiwa kuwaangalia watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu, pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo, ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita kiasi.
“Vilevile Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo,” alisema Sirro.
|
0 Comments