Mwanasiasa wa upinzani Kenya aliyeidhinisha kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi' Januari Miguna Miguna ametimuliwa tena kutoka nchini humo.
Mwanasiasa huyo ametimuliwa huku mzozo kuhusu uraia wake ukiendelea.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Mawakili wa Bw Miguna wamethibitisha kwamba aliondolewa nchini humo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai.
Bw Miguna alikuwa amezuiliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) tangu alipowasili Jumatatu adhuhuri.
Mwanasiasa huyo alikuwa anajaribu kurejea kutoka Canada ambako alikuwa amepelekwa baada ya kufurushwa kutoka Kenya kwa lazima mwezi Februari.
Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga Jumatano alisema waziri wa usalama nchini humo, mkuu wa polisi na mkuu wa idara ya uhamiaji watakuwa wamekaidi maagizo ya mahakama iwapo wangekataa kumwachilia huru.
Alikuwa ametoa ilani kwa watatu hao kufika mahakamani baadaye Jumatano lakini baada yao kukosa kufika akawapata na hatia ya kukaidi agizo la mahakama.
Aliahidi kutoa adhabu dhidi yao leo asubuhi.
Maafisa wa Kenya mnamo 6 Febuari walikuwa wamemfukuza kutoka nchini humo kutokana na mchango wake wakati wa kuapishwa kwa Bw Odinga.
Walisema mwanasiasa huyo hana uraia wa Kenya lakini ana uraia wa Canada.
Idara ya uhamiaji ya Kenya imekariri kuwa Miguna alipoteza uraia wa Kenya mwaka 1998 alipopewa uraia wa Canada wakati ilipokuwa ni kinyume cha sheria kuwa na uraia wa nchi mbili nchini Kenya.
Kuzuiliwa kwa Bw Miguna kumejadiliwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii Kenya, baadhi wakiunga mkono hatua hiyo lakini wengine wakiwashutumu maafisa wa uwanja wa ndege na serikali.
Kukamatwa kwa Miguna mara ya kwanza
Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "Rais wa Wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.
Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.
Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.
Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.
Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba na kutangaza kwamba hakumtambua Bw Kenyatta kama rais halali wa nchi hiyo.
Baadaye aliongoza hafla ya kuapishwa kwake mnamo tarehe 30 Januari.
Mapema mwezi huu, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta walikutana katika mkutano ambao haukuwa umetarajiwa na wakahutubia wananchi moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.
Waliahidi maridhiano na pia wakaahidi kuwaunganisha tena Wakenya.
Bw Miguna mnamo Jumatano alikuwa ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumanne kwamba alikuwa anazuiliwa chooni uwanja wa ndege na kwamba alikuwa amezuiwa kuwaona mawakili wake na jamaa zake.
0 Comments