WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amebainisha mkakati wa serikali wa kupunguza maeneo ya hifadhi na kupeleka kwa wananchi, ikiwa ni njia ya kupunguza migogoro ya mipaka.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeiagiza serikali iwasilishe ripoti nne kuhusu sheria, utalii wa uwindaji wa kitalii, migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji na faida na hasara za kodi katika sekta hiyo, ambayo imetakiwa kuifikia Kamati kabla ya kusomwa kwa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18, Dk Kigwangalla amesema, amefikia hatua hiyo hasa kutokana na migogoro kuzidi kutokana na wananchi kuhitaji ardhi, huku wengine wakiwa na tafsiri tofauti ya mipaka kati ya kijiji na hifadhi.
"Mfano wilaya ya Kaliua, asilimia 95 ni hifadhi, na asilimia tano ndiyo ya wananchi, maeneo kama haya na mengineo tunafanya utaratibu wa kupunguza maeneo ya hifadhi na kuwaongezea wananchi ardhi, lakini wakati huo huo, tunatafuta maeneo mengine ya hifadhi ili kufidia," amesema.
Aidha, alisema malalamiko ya wananchi wanaoingiza mifugo kwenye hifadhi, yanakuwa magumu kuyatatua kutokana na sheria zilizopo, ambapo mifugo inayoingia kwenye mbuga za wanyama hutozwa faini ya kati ya Sh 1 hadi 100,000 kwa mfugo, wakati ile inayoingizwa kwenye hifadhi kesi haye huamriwa na mamlaka nyingine.
Akitoa hitimisho baada ya kikao hicho, Mwenyekiti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii, Nape Nnauye aliiagiza wizara hiyo kuwasilisha kwa kamati hiyo ripoti kuhusu sheria ambazo zimepitwa na wakati na zinakwaza maendeleo ya sekta ya utalii ili Bunge iziboreshe Kamati pia iliagiza wizara kuwasilisha ripoti, inayohusu migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji.
Pia iliitaka wizara kuja na ripoti ya uchambuzi wa kina wa matokeo ya kodi iliyowekwa kwenye sekta ya utalii baada ya kubainika sekta hiyo kuwa na kodi zaidi ya 31.
Kamati ilitaka ripoti iwafikie kabla ya kusomwa kwa bajeti ya wizara husika. Kuhusu sekta ya uwindaji wa kitalii, kamati ilitaka serikali kuja na ripoti inayokamilikia, ikiwa na takwimu ikionesha hali halisi ya vitalu ikoje.