UBALOZI wa China nchini kwa kushirikiana na wizara inayosimamia sekta ya kilimo Zanzibar, wanatarajiwa kuzindua maonesho ya kilimo yatakayoanza Aprili 9, mwaka huu, katika Bonde la Cheju mkoani Kusini Unguja kwa lengo la kuwaandaa wakulima kuendesha kilimo katika njia na misingi ya teknolojia ya kisasa.

Maonesho hayo yatakwenda sambamba na ubalozi wa China nchini kugawa vifaa vya kilimo kwa wakulima wa Zanzibar ambapo wataalamu watakaosimamia maonesho hayo wanatarajiwa kuingia nchini wakati wowote kuanzia leo.
Balozi Mdogo wa China, Zanzibar, Xie Xiaolon amesema hayo wakati akitoa taarifa kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake Vuga.
Balozi Xiaolon alisema Zanzibar ni miongoni mwa maeneo mengi yaliyotengwa nchini Tanzania yatakayofaidika na mpango wa upandaji bora wa mpunga kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambao utatolewa ufafanuzi katika maonesho hayo.
Amesema hatua ya kuandaliwa kwa maonesho hayo imetokana na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania, ikiwemo Zanzibar kwa ujumla hasa katika nyanja za kilimo na maeneo mengine ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Alieleza kuwa utafiti uliofanywa kupitia mpango huo wa upandaji wa mpunga kwa kutumia njia na mfumo wa teknolojia ya kisasa, unawezesha ekari moja kutoa zaidi ya tani saba hadi tisa za mpunga, jambo ambalo linaweza kuleta ustawi wa haraka kwa wakulima wa Zanzibar.
Balozi Iddi alisema maonesho hayo yatasaidia wananchi walio wengi hapa nchini.
Alisema wananchi wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba wanaishi vijijini na mategemeo yao makubwa katika kujipatia riziki na maendeleo yao yanatokana na sekta mama ya kilimo.
Aliipongeza China kwa juhudi inayoendelea kuchukua kwa kusaidia ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kiuchumi akitolea mfano mradi wa ujenzi wa shule ya Pangawe, ujenzi wa uwanja wa michezo ya Mao Tse Tung uliopo Mperani Kikwajuni pamoja na ukamilishaji wa jengo la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.
Akizungumzia sekta ya uvuvi wa bahari kuu, Balozi Iddi alisema China imeonesha nia ya kutaka kusaidia sekta hiyo muhimu kutokana na Visiwa vya Zanzibar kuzungukwa na bahari katika maeneo yake yote.
Balozi Seif alisema kitendo cha China kukubali kuwagharamia baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupata mafunzo na fursa mbalimbali za kitaalamu zinazotokana na sekta hiyo nchini China ni mwanzo mzuri wa kufungua milango ya uwekezaji katika eneo hilo pana la uvuvi.