RAIS John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kutokana na ajali iliyoua watu 26 wakiwemo watoto saba.
Watu hao walikufa jana usiku wakati lori lilipogongana na basi dogo la abiria kwenye Kijiji cha Kitonga, kata ya Mwalusembe wilayani Mkuranga, Pwani.

“Nimesikitishwa sana na taarifa ya vifo vya watu 26 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea huko Mkuranga mkoani Pwani, tumepoteza idadi kubwa ya Watanzania wenzetu na nguvu kazi ya Taifa.
“Naungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao na watu waliowategemea,” imesema sehemu ya salamu hizo za Rais Magufuli.
Rais Magufuli amemtaka Ndikilo afikishe salamu za pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na pia amevitaka vyombo vinavyoshughulikia usalama wa barabarani kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.
Amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na majeruhi tisa wa ajali hiyo wapone haraka ili waungane na familia na jamaa zao kuendelea na shughuli za kila siku.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Muslimu amesema ajali ilitokea saa tatu usiku ikihusisha magari mawili likiwemo lori aina ya Scania lenye namba za usajili T223 CZB lililokuwa na tela lenye namba za usajili T371 CBT na Toyota Hiace yenye namba za sajili T676 DGK.
Lori hilo lilikuwa limebeba mifuko ya chumvi likitoka mkoani Lindi kwenda jijini Dares Salaam.
Basi dogo lilikuwa linatoka Mbagala kwenda Kimanzichana. Watu wanane walijeruhiwa na wanapatiwa tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda Muslimu, dereva wa lori, bila tahadhari alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi katika eneo hilo ambalo kuna mteremko na kona hivyo gari likamshinda, likahama kutoka kushoto kwenda kulia na kugonganana na basi dogo lililokuwa limebeba abiria.
Amesema katika ajali hiyo wamekufa wanawake 12, wanaume saba, na watoto saba wanaokisiwa kuwa na umri kuanzia mwaka mmoja hadi minne. Dereva wa lori anapatiwa tiba chini ya ulinzi.