WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani, amesema baada ya miezi mitatu, serikali itatoa uamuzi kama nchi iendelee kutumia mita za umeme zinazotengenezwa nje ya nchi au kupiga marufuku uingizaji wa mita hizo.
Itafanya hivyo baada ya kujiridhisha na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha mita husika.
Dk Kalemani alisema hayo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme, lengo likiwa ni kujiridhisha na uwezo wa kiwanda hicho katika kukidhi mahitaji ya mita nchini.
"Serikali imeweka miezi mitatu ya matazamio ili kuona kama viwanda vyetu ambavyo sasa ni viwili, vina uwezo wa kuzalisha mita za umeme za kutosha na zenye ubora zitakazokidhi soko la ndani kisha tutatoa uamuzi kuhusu uingizaji wa mita hizo nchini," alisema Dk Kalemani.
Miezi kadhaa iliyopita, serikali ilitoa katazo la kuagiza nguzo za umeme na transfoma kutoka nje ya nchi, baada ya kujiridhisha kuwa uwezo wa kuzalisha vifaa hivyo unajitosheleza.
“Sasa katika mita hizi za umeme pia tunafanya ukaguzi ili kujiridhisha na uwezo wetu," aliongeza.
Alisema uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini una faida mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za usafirishaji, mita kupatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa wingi.
"Mfano gharama ya mita moja ya njia moja ya umeme kutoka nje ya nchi ni Sh 150,000 na njia tatu za umeme ni mpaka Sh 700,000 lakini mita zinazozalishwa nchini unazipata si kwa zaidi ya Sh 120,000 kwa mita za njia moja ya umeme na haizidi Sh 450,000 kwa mita za njia tatu za umeme," alisema.
Awali Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha Baobab, Hashim Ibrahim, alimweleza Dk Kalemani kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mita 38,000 kwa mwezi na kwa mwaka wanazalisha mita 456,000.
Aliongeza kuwa, mita hizo zina faida mbalimbali ikiwemo kuwa na mfumo wenye uwezo wa kuzuia matukio ya wizi wa umeme kwa asilimia 99 na kudhibiti upotevu wa umeme.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Mauzo na Masoko wa Shirika hilo, Theodory Bayona, alisema mahitaji ya shirika hilo ni mita 20,000 kwa mwezi, ambapo kati ya hizo, mita 1,000 ni za njia tatu za umeme. Kiasi hicho cha mita ni kwa ajili ya wateja wapya.
|
0 Comments