RAIS John Magufuli amezindua magari 181 ya Bohari ya Dawa nchini (MSD) yatakayotumika kusambaza dawa na vifaa tiba kote nchini.
Ameyazindua leo kwenye Viwanja vya makao makuu ya MSD Keko jijini Dar es Salaam.
Magari hayo ni msaada uliotolewa na taasisi ya Global Fund yakiwemo magari madogo aina ya Toyota LandCruiser 104 na malori 77 aina ya MAN yaliyotengenezwa Ujerumani ambayo yako kwenye uzito tofauti.
Malori 10 kati ya hayo yana uzito wa tani 15, 11 yana uzito wa tani 10 na malori 56 yana uzito wa tani 5.5.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema, magari hayo yamesajiliwa kwa namba za Serikali za ‘SU’kwa kuwa yametolewa bila masharti yoyote.
Amesema magari hayo yatasaidia kusambaza madawa hadi kwenye milango ya vituo vya kutolea huduma za afya kila mahali nchini.
Endapo magari hayo 181 yatagawanywa kwa uwiano sawa katika Kanda nane za MSD ambazo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tabora, Moshi, Iringa, Dodoma na Mtwara, basi kila Kanda itapata mgawo wa wastani wa magari 23 na kwa upande wa mikoa 25 ya Tanzania Bara, kila mkoa utapata mgawo wa wastani wa magari 7.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, magari hayo ambayo ni msaada kutoka Mfuko wa Pamoja (Global Fund) yana thamani ya Sh bilioni 20.75.
Amesema, Mfuko huo wa Pamoja umesaidia kupunguza changamoto ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini kwa kuwa hivi sasa MSD itakuwa na jumla ya magari 213 kutoka magari 32 iliyokuwa nayo awali.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa Mfuko wa Pamoja (Global Fund) kutupatia msaada. Tangu Mfuko huo uanzishwe mwaka 2003 hadi kufikia Julai 2017, nchi yetu ilikuwa inanufaika na msaada wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.9 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh trilioni 4,”alieleza Dk Magufuli.
|
0 Comments