WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesifu utendaji kazi na uwekezaji uliofanyika katika kiwanda cha maziwa kinachomilikiwa na kampuni ya Azam, kilichopo Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi na kusema kinaweza kuingia katika ushindani wa soko la Afrika ya Mashariki.
Mwijage amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho ambapo alisema amefurahishwa na mitambo ya kisasa ya uzalishaji wa maziwa yenye ubora wa hali ya juu.
Amesema ili viwanda vya Tanzania vifanikiwe kuingia katika soko la ushindani la Afrika ya Mashariki suala la ubora wa uzalishaji wa bidhaa za viwango ni muhimu.
Aidha, Mwijage ameushauri uongozi wa kiwanda hicho kuzalisha na kutengeneza maziwa halisi ya ng’ombe yatakayosaidia wafugaji kuongeza uzalishaji na kutosheleza soko la Tanzania.
Kwa mfano amesema, kiwanda cha maziwa kilichopo Tanga kimesaidia na kuamsha ari kwa wafugaji wa ng’ombe kuzalisha bidhaa ya maziwa.
Alimtaka mwekezaji wa kiwanda cha maziwa cha Azam kilichopo Fumba kuwahamasisha wafugaji kuongeza ari ya kufuga ng’ombe kwa ajili ya kupata maziwa kwa wingi.
“Nimekitembelea kiwanda cha maziwa na kubaini kwamba hakitengenezi maziwa halisi ya ng’ombe na hiyo inatokana na ukosefu wa malighafi ya maziwa ...huu ni wakati muafaka wa kuwahamasisha wafugaji kuongeza uzalishaji wa maziwa ya ng’ombe,” amesema.
Mapema Mwijage aliwataka wafanyabiashara na wazalishaji wa viwanda kuongeza ubora wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la Afrika ya Mashariki na nje ya mipaka hiyo.
Amesema, ubora wa bidhaa unaozingatia viwango ndiyo silaha kubwa ambayo itawawezesha wafanyabiashara kuingia katika soko la Afrika ya Mashariki kwa ushindani.
“Serikali siku zote inasisitiza na kuwataka wafanyabiashara kuzingatia ubora wa bidhaa zao wanazozalisha ili ziweze kuingia katika ushindani wa soko,” amesema.
Mwijage alikuwa Zanzibar mwishoni mwa wiki na kuzungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Waziri Balozi Amina Salum Ali.
|
0 Comments