Nyimbo mbili za Diamond Platnamz ni miongoni mwa nyimbo zaidi ya 10 zilizopigwa marufuku kupigwa katika radio nchini Tanzania.
Nyimbo kadha za wanamuziki Ney wa Mitego, Roma Mkatoliki, Jux na Barnaba pia zimefungiwa.
Nyimbo za Diamond, ambaye jina lake halsii ni Nasib Abdul, zilizofungiwa ni Hallelujah (uliomshirikisha Morgan Heritage ) na Waka Waka (uliomshirikisha Rick Ross).
Barua kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania kuelekea Radio moja mjini Dodoma imesema nyimbo hizo zimefungiwa kwa ushauri kutoka kwa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Basata wamewasilisha kwa TCRA orodha ya nyimbo hizo ambazo zimedaiwa kuwa "zisizokuwa na maadili."
"Nyimbo hizo zilitolewa na wasanii na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya utangazaji na mitandao ya kijamii," taarifa a TCRA imesema.
"Nyimbo hizo zina maudhui ambayo ni kinyume na maadili na Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005."
Nyimbo mbili za Ney wa Mitego, jina lake halisi Emmanuel Elibariki - Pale kati Patamu na Maku Makuz - pia zimefungiwa.
Mwanamuziki Roma Mkatoliki ambaye jina lake halisi ni Abernego Damiani naye amefungiwa wimbo wa Kibamia.
Wimbo wa Amani Hamisi maarufu kama Manifango wa Hainaga Ushemeji pia umefungiwa, sawa na I am Sorry JK wake Nikki Mbishi ambaye jina lake halisi ni Nicas John Mchuche.
Snura Mushi ambaye jina lake la usanii ni Snura amefungiwa nyimbo mbili - Chura na Nimevurugwa.
Nyimbo nyingine ni Tema mate tumchape (Hamad Ali maarufu Madee), Uzuri Wako (Juma Mussa Mpolopoto maarufu Jux), Nampa Papa (Gift Stanford maarufu Gigy Money) na Nampaga (Barnaba Elias maarufu Barnaba).
Mwana 2016, TCRA walikuwa wameufungia wimbo wa Chura wake Snura.
Baadaye aliomba radhi na kuahidi kutekeleza maagizo ya serikali.
Hata hivyo, bado ametetea video zilizotolewa za wimbo huo akisema zilitolewa tu kwa ajili ya YouTube.
0 Comments