WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kuchunguza na kufanya utafiti ili kubaini kwa nini mkoa wa Dodoma, ambao kwa sasa ni makao makuu ya nchi, unafanya vibaya katika elimu.
Ametoa agizo hilo wakati anafungua mkutano wa Maofisa Elimu wa Wilaya na Mikoa Alisema kuna haja ya Mkoa wa Dodoma kuchunguzwa kwa nini unafanya vibaya katika elimu.
“Naibu Katibu Mkuu uchunguze Mkoa wa Dodoma haiwezekani miaka nenda rudi haujawahi kufanya vizuri, bado tia maji tia maji kuna mdudu gani anasababisha hali hii, unaweza kuwasulubu maofisa elimu kumbe chanzo kinaweza kuwa ni tofauti,” amesema.
Aidha, Jafo amesema kama kungekuwa na uwajibikaji wa kweli, ufaulu ungefikia asilimia 80.
Amesem, kuna haja ya kuzifanyia kazi changamoto zote, ambapo sasa madarasa yaliyopo ni aslimia 52.8 na upungufu huo umetokea baada ya Rais John Magufuli kuweka sera ya kutoa elimu bila malipo hali iliyoongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shule.
Alisema hali si mbaya kwa upande wa shule za sekondari madarasa yanayotakiwa ni 39,940, sawa na asilimia 98.8 wakati waliyopo ni 39,490.
Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe amewataka maofisa elimu kuanzia ngazi ya kata hadi mikoa kuacha kuwatesa walimu ambao wamekuwa wakijazana wizarani kuonana na viongozi na kufanya korido za wizara kuwa kama wodi za wagonjwa.
Amesema sasa ni wakati wa maofisa elimu hao kujitathimini kama wanatosha na kama wanaweza kuongoza walimu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amewataka maofisa hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
|
0 Comments