JUKWAA la fursa ya biashara Zanzibar linaloandaliwa na Kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) lina lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika visiwani humo.
Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi amesema mjini Zanzibar kuwa, jukwaa hilo litaibua fursa zilizopo visiwani humo ambazo hazifahamiki na kwamba, zaidi ya watu 400 wamethibitisha kushiriki.

Majukwaa ya biashara yanayoandaliwa na TSN yalianza Februari mwaka jana mkoani Simiyu, na litakalofanyika Zanzibar Machi 15 mwaka huu litakuwa la tano.
Kwa mujibu wa Dk. Yonazi jukwaa la Zanzibar litasaidia kuifahamisha dunia fursa zilizopo Zanzibar na namna visiwa hivyo vilivyo tayari kutekeleza azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.
Dk Yonazi ametoa mfano wa sekta ya utalii ambayo ni maarufu katika visiwa hivyo jukwaa hilo litaibua fursa za utalii ili kuongeza mapato ya wananchi na Serikali.
Jukwaa hilo la kwanza kwa mwaka huu, mengine yamefanyika Mwanza, Tanga, na Shinyanga.