WANANCHI 87 kwenye vijiji vya mkoani Kusini Unguja wamejiajiri kwa kufuga vipepeo na kuuza buu kwenye Kituo Cha Vipepeo Zanzibar (ZBC).
Mratibu wageni ZBC, Omary Mzee Khamis amesema, buu ni kama mdudu anayetokana na funza alizaliwa kutoka kwenye yai la kipepeo, na hatimaye hutunzwa kituoni hapo ili kupata kipepeo mwingine.

Wananchi hasa kwenye Kijiji cha Pete wanapouza buu hao wanajipatia takribani shilingi 400,000 kila baada ya wiki mbili.
ZBC inanunua buu kwa kati ya shilingi 100 hadi 800 kwa kuzingatia ni aina gani ya vipepeo.
ZBC inawawezesha wananchi kuanzisha miradi hiyo kwa kuwapatia vifaa vinavyogharimu shilingi 200,000/- Utalii ulianzishwa kwenye eneo hilo mwaka 2007 baada ya mtalii raia wa Scotland kufika kwenye hifadhi ya Taifa ya Jozani Ghuba ya Chwaka na kufanya utafiti kwa nini wananchi wa maeneo hayo wanaharibu mazingira ya hifadhi hiyo na kubaini kuwa wanafanya hivyo kutokana umasikini.
Mtalii Benjamini Heys alitoa mafunzo kwa wakazi watano wa eneo hilo wanaosimamia kituo hicho hivi sasa.
Khamis amesema, ZBC ina aina 25 ya vipepeo ikiwemo moja inayopatikana Zanzibar pekee Kwa mujibu wa Khamis, kila mwaka ZBC inapata takribani watalii 5,000 wanaopatia kituo shilingi milioni tano hadi sita kila mwezi.
Raia wa nje wanaotembelea eneo hilo wanalipa wanalipa Dola sita za Marekani sawa na shilingi 12,000 za Tanzania.