Barcelona imesalia na ushindi mmoja pekee kujipatia taji la 25 la ligi ya La Liga baada ya Atletico Madrid kupoteza kwa Real Sociedad.
Kikosi hicho cha Diego Simeone hakikuonyesha mchezo mzuri na kikajipata nyuma wakati Willian Jose alipomaliza pasi iliopigwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Adnan Januzaj.

Mchezaji wa ziada Juanmi alifunga bao la pili katika saa za lala salama kabla ya kuongeza bao lake la pili katika dakika ya mwisho.
Barcelona sasa itashinda taji la La Liga iwapo itashinda mechi yake dhidi ya Deportivo Lacuruna tarehe 29 Aprili.
Barca ilimaliza ya pili msimu uliopita wakiwa pointi tatu nyuma ya mabingwa watetezi Real Madrid.
Atletico ambao wako pointi 12 nyuma ya Barcelona wanaelekea Arsenal katika awamu ya kwanza ya mechi ya nusu fainali ya kombe la Yuropa tarehe 26 Aprili.