WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto imesema, asilimia 27 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 aidha wana watoto au ni wajawazito.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Faustine Ndungulile amesema, katika baadhi ya mikoa karibu asilimia 57 ya wenye umri huo ni wajawazito au wana watoto.
Ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati anajibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum, Aisharose Matembe Amesema, Serikali inatambua kuna changamoto kubwa ya mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa Dk. Ndungulile, kuna kampeni iliyoanzishwa yenye kauli mbiu ‘Mimi ni msichana, najitambua, elimu ndiyo mpango mzima’. Amesema, pia zimeanzishwa klabu zinazoelimisha mabinti kujitambua ikiwa ni pamoja na kupata elimu ya uzazi.
Ndungulile pia amesema, Serikali imeongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi bilioni tano hadi bilioni 18.
Ameagiza waganga wakuu wa mikoa na waganga wakuu wa wilaya waagize dawa na vifaa tiba kwa ajili ya masuala ya uzazi wa mpango.
Katika swali la msingi, Matembe aliuliza Serikali ina mkakati gani kuimarisha huduma za afya ya uzazi wa mpango mkoani Singida kwa kuwa, utumiaji wa huduma hizo ni asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni 27%.
Wakati wa swali la nyongeza Mbunge huyo aliuliza Serikali haioni ni muhimu kuwa na kampeni ya kitaifa hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kupambana na mimba za utotoni.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile amesema, serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu uzazi wa mpango kwa kutumia simu za mkononi na kwamba, wananchi wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wanaweza kupata ujumbe wenye elimu ya uzazi wa mpango.
“Katika Mkoa wa Singida wateja waliopatiwa huduma ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2015 walikuwa 198,822, mwaka 2016 walikuwa wateja 209, 511 na mwaka 2017 walikuwa wateja 173,587.” amesema Ngungulile.
Amesema, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya afya, wameshirikiana na mkoa wa Singida kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma 77 kwa kipindi cha mwaka 2015 na mwaka 2016 idadi ilikuwa 121.
|
0 Comments