Maafisa watatu wakuu wa tume ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC) akiwemo naibu mwenyekiti wamejiuzulu wakidai kutokuwa na imani na mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati.
Makamishna hao wamedai kuwa bodi hiyo imeshindwa kutimiza wajibu na imeeingiliwa na watu wengine.
Wakihutubia wanahabari jijini Nairobi, makamishna hao Consolata Nkatha, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya wamedai kuwa Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ameshindwa kuiongoza tume hiyo na kudai kwamba tume hiyo imeingiliwa na watu kutoka nje wanaoshawishi jinsi inavyofanya kazi.
''Kwa muda murefu sasa, mwenyekiti ameshindwa kutoa muongozo wa utaratibu kwa wakati mgumu na anapohitajika kufanya hivo.
Katika taarifa yake hivi punde kwa waandishi wa habari, mwenyekiti wa tume hiyo ya IEBC - Wafula Chebukati amesema kwamba hakujakuwa na mawasiliano rasmi kuhusu kujiuzulu kwa makamishna hao watatu na kwamba amepata kusikia kuhusu taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari nchini.
Badala yake, chini ya uongozi wake, bodi ya tume imegeuzwa kuwa sehemu ya kusambaza habari zisizo sahihi, kukuza kutoaminiana na kutengeneza nafasi ya kung'angania sifa.
Kutokana na hilo, tunajutia kutangaza kujiuzulu kutoka kwa tume mara moja.'' amesema Margaret Mwachanya, Kamishna wa IEBC.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika ujumbe kwa vyombo vya habari amekana kujulishwa kuhusu uamuzi wa makamishna hao na kudai alipata habari kupitia vyombo vya habari .
Uamuzi wa kujiuzulu kwao unajiri wiki moja tu baada ya mwenyekiti Wafula Chebukati kumsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji Ezra Chiloba kutokana na madai ya kuhusika na kashfa ya ununuzi wa baadhi ya vifaa vya utendaji kazi katika tume hiyo.
Kujiuzulu kwa makimishna wa IEBC ina maana gani?
Tume hiyo ya makamishna saba sasa imesalia na watatu tu baada watatu kuondoka hii leo.
Kwa jumla makamishna waliondoka ni zaidi ya nusu.
Kuondoka kwao sasa kunaacha tume hiyo bila idadi ya makamishna inayohitajika kisheria kutimiza wajibu wake hadi ivunjiliwe mbali na tume mpya kuundwa.
Tume hiyo imekumbwa na msukosuko na kujiwekea rekodi ya aina yake.
Mahakama ya juu zaidi ilifutilia mbali uchaguzi uliyosimamiwa na tume hiyo.
Kisha upinzani nchini Kenya ukiongozwa na kinara Raila Odinga ukaususia uchaguzi wa marudio ukitaka tume hiyo kuvunjiliwa mbali.
Hilo halikufanyika na rais Uhuru Kenyatta akatangazwa mshindi wa kura hizo kwa asilimia kubwa.
Hata hivyo upinzani ulizidi kushikilia tume hiyo ivunjwe hata baada ya uchaguzi lakini serikali ikapinga.
Kujiuzulu kwa makamishna hao sasa bila shaka kunaongeza joto kwa mjadala wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
|
0 Comments