MJI wa serikali wa kwanza na wa aina yake nchini utajengwa mjini Dodoma na utagharimu Dola za Marekani bilioni 4.8 sawa Sh trilioni 10.7.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi amewaeleza waandishi wa habari kuwa, ujenzi wa mji huo utakamilika ndani ya miaka 10.
Kunambi amesema Manispaa ya Dodoma imetenga eneo utakapojengwa Mji wa Serikali, lenye ukubwa wa hekta 617.15 sawa na ekari 1,542.88 katika Kata ya Ihumwa kilomita 17 kutoka katikati ya mji huo.
Kwa mujibu wa Kunambi, upande wa magharibi eneo hilo linapakana na kambi ya Jeshi ya Ihumwa, kaskazini mashariki linapakana na kata ya Mtumba na kusini linapakana na barabara iendayo Dar es Salaam.
Pia amesema Manispaa ya Dodoma imepima viwanja 1,288 vyenye ukubwa mbalimbali katika eneo hilo, na kwamba, mji wa serikali una viwanja 147 ambavyo kati yake, viwanja vya wizara ni 33 na vya mabalozi ni 64.
"Pia kuna viwanja vingine 50 ambavyo vimetengwa kwa matumizi mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kibiashara," amesema Kunambi.
Kunambi amesema fedha za ujenzi wa mji huo zinatarajiwa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo serikali kuu, wafadhili, mashirika ya umma, taasisi binafsi na za serikali na mashirika binafsi.
Amesema mji huo wa serikali utakuwa pia na taa za barabarani, barabara za mitaa na sehemu za mapumziko. Kunambi alisema mji huo wa serikali utakuwa unatumia maji lita za ujazo 3,016.7 kwa siku katika shughuli zake.
"Pia mfumo wa maji taka utakuwa umeunganishwa wa kisasa ambao utakuwa unafanya kazi ya kupokea majitaka na kuyachakata na kuwa majisafi tena kwa matumizi mengine," amesema.
Kunambi amesema mfumo huo, utakuwa wa kisasa kama unavyoonekana hapo chini. Pia usafiri wake utakuwa wa bei nafuu, sehemu za watembea kwa miguu pamoja na usafiri wa treni.
Pia alisema pamoja na kupima viwanja vya mji wa serikali, Manispaa hiyo pia imepima viwanja 922 katika eneo la Nala, pia imepima Kiwanja cha Kimataifa cha Michezo kilichopo Nzuguni na maeneo mengine yenye viwanja 218.
|
0 Comments