Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema, mwanadamu si jiwe hivyo lazima apite kwenye mapito.
Amesema, kila mtu lazima apite kwenye mapito na kwamba, hata hali ya yeye kuumwa ni mapito.
"Ukiupata msalaba ubebe kwa amani" amesema Spika Ndugai bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Ameomba msalaba wake usiwe mzito sana, uwe wa kadiri tu.
Amemshukuru Mungu kwa kumponya na kumrudisha salama bungeni kuendelea na majukumu yake.
Ameshukuru sala, dua za Watanzania waliomuombea wakiwemo wapiga kura katika Jimbo la Kongwa.
Amemshukuru Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson , wenyeviti wa Bunge, Andrew Chenge, Musa Azzan Zungu, Najma Murtza Giga, Katibu wa Bunge na timu yake kwa kuwa wamefanya kazi kubwa wakati yeye akiendelea na tiba.
Ndugai pia amemshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kumtia moyo wakati alipokuwa kitandani akiumwa.
Kwa mujibu wa Ndugai, kuna wakati mtu anajiona mpweke, anaona dalili kwamba huenda kesho haitafika na haombei wabunge wapitie machungu hayo.
Wabunge wakiwemo viongozi wa Serikali wamemkaribisha Spika Ndugai na wamemweleza walikuwa wamemkumbuka.
|
0 Comments