WIZARA ya Fedha na Mipango imelieleza Bunge kuwa, Kiwanda cha Sukari Kagera kimekopa Dola za Marekani milioni 65 kwa guarantee ya Serikali.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Ashatu Kijaji ameyasema hayo bungeni wakati anajibu swali la Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa.
Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali ina hisa kiasi gani kwenye Kiwanda cha Sukari Kagera na ni kiasi gani cha fedha amekopa mwekezaji kwa guarantee ya Serikali.
"Kwa sasa Serikali haimiliki hisa katika kiwanda cha sukari cha Kagera (Kagera Sugar Company Ltd). Serikali kupitia PSRC ilibinafsisha kiwanda hicho kwa kampuni ya Kagera Saw Mills Limited kwa kuuza hisa zake zote mnamo mwaka 2001" amesema Dk. Kijaji.
Amesema, Kagera Sugar Company Ltd walichukua mkopo huo mwaka 2004 kwa guarantee ya miaka 12. "Hadi sasa zaidi ya Dola za Marekani milioni 56.88 zimerejeshwa, sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote. Aidha, marejesho ya sehemu ya mkopo uliobaki wa Dola za Kimarekani milioni 8.12 yatafikia ukomo wake mwezi Julai, 2019" amesema Dk. Kijaji.
Kwa mujibu wa Dk. Kijaji, kiwanda cha sukari cha Kagera kimewekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 250 na ni miongoni mwa viwanda vinavyofanya vizuri Tanzania.
Amesema, wawekezaji kwenye kiwanda hivyo wasikatishwe tamaa, wapewe moyo ili wafanye vizuri.
Ameyasema hayo baada ya Mbunge Mchengerwa kuuliza kwa nini mwekezaji amekopa kwa guarantee ya Serikali halafu anawekeza DRC Congo wakati bado kuna mahitaji ya sukari nchini.
Amewaeleza wabunge kuwa, Serikali ipo kwenye mchakato wa kukiendeeleza kiwanda hicho ili kuongeza tija.
Dk Kijaji amesema, kiwanda cha sukari cha Kagera kinatoa ajira kwa wananchi, elimu kwa watoto wa wafanyakazi na huduma za afya kwa wananchi.
Wakati anatoa nyongeza ya majibu ya serikali, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amesema, haijawahi kutoa kibali kwa kiwanda cha sukari Kagera kupeleka sukari nje ya nchini.
|
0 Comments