|
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepanga kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa ili kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi na zimetengwa Sh bilioni 40.7 kwa matibabu hayo.
Hayo yamesemwa na Waziri Ummy Mwalimu, alipowasilisha makadirio ya matumizi ya bajeti ya Sh bilioni 898.4 kwa mwaka wa fedha 2018/19, bungeni mjini Dodoma jana. Bajeti hiyo ni pungufu kwa asilimia 19.6 kutoka Sh trilioni 1.1 zilizoombwa kwa mwaka wa fedha 2017/18. Ummy alisema vipaumbele ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa nchi nzima. Waziri huyo alisema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini kwa kununua na kuvisambaza katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya, zimetengwa Sh bilioni 270 na magari ya wagonjwa 27 yamepangwa kununuliwa.
Akitoa mchanganuo uimarishwaji wa matibabu ya kibingwa, Ummy alisema Sh bilioni 16 zimetengwa kujenga jengo maalumu kwa wagonjwa wanaolipia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Sh bilioni 4.2 kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa kugharamia vipandikizi katika Taasisi ya Mifupa (MOI). Pia Sh bilioni 14.5 kwa ajili ya kununua na kusimamia vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ikiwa ni pamoja na PET Scan, Sh bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Sh bilioni 1 kwa ajili ya Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara.
Ummy alisema pia serikali imetenga Sh bilioni 30 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, kwa ukarabati wa miundombinu, kuanzisha na kuboresha vitengo vya dharura na ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa katika mikoa ya Katavi, Njombe, Geita, Simiyu, Songwe na Mara. Kuhusu uhakiki wa ubora wa huduma za afya, Ummy alisema wizara imekamilisha Mwongozo wa viwango vya misingi kwa vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambao utaanza kutumika mwaka 2018/19.
“ Wizara itafanya tathimini ya ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na kuvipa hadhi stahiki,” alisema. Akibainisha vipaumbele vya Idara ya Maendeleo ya Jamii, waziri huyo alisema kwa mwaka wa fedha 2018/19, wizara itawezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017 hadi 2022 ili kupunguza ukatili dhidi yao kwa asilimi 50. Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba aliitaka serikali itoe fedha kwa wakati na kama zilizovyoombwa ili kuweza kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa mwaka 2018/19.
0 Comments