WAFANYAKAZI wawili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameunganishwa na wenzao watatu akiwemo aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi wanaokabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha.
Washitakiwa hao ni Meneja wa Ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Aidha, mahakama hiyo imepanga kuanza kusikiliza mfululizo kesi hiyo kuanzia Mei 14,17 na 21 mwaka huu.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai aliomba mahakama kufanya mabadiliko ya hati ya mashitaka na kusoma mashitaka hayo upya ambayo yamefika 30 badala ya 28 ya awali.
Mbali na Malinzi (57) wengine kwenye kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27).
Akisoma mashitaka hayo, Swai alidai Malinzi anakabiliwa na mashitaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh milioni 43.1.
Pia alidai mshitakiwa Mwesigwa anakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji fedha hizo.
Mshitakiwa Nsiande anakabiliwa na mashitaka mawili ya utakatishaji fedha, huku washitakiwa hao wapya Zayumba na Rauya wakikabiliwa na mashitaka 10 ya kughushi nyaraka.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na upande wa jamhuri ulieleza kuwa upelelezi umekamilika na wako tayari kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao.
Swai aliwasomea washitakiwa maelezo ya awali ambapo walikubaliana na maelezo yao binafsi, ikiwemo majina, nafasi za kazi, umri na kukana maelezo ya mashitaka.
Washitakiwa walifanikiwa kupata masharti ya dhamana kwa sababu mashitaka ya kughushi yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Mashauri alimtaka mshitakiwa Rauya kuwa na wadhamini 2 ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 20 na Zayumba alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 100 kila mmoja.
Mshitakiwa Rauya alifanikiwa kupata dhamana lakini Zayumba hakupata hivyo alipelekwa mahabusu na Malinzi na wenzake.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza.
|
0 Comments