SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amezuia wabunge wasiingie au kutumia na vifaa vya kielektroniki vya kuhifadhia nguvu ya betri ya simu (power bank) na chaja za simu ndani ya ukumbi wa Bunge.
Amesema, wamepokea ushauri kutoka vyombo vya ulinzi na usalama kwamba wakati uchunguzi wa tukio la kulipuka power bank unaendelea, wabunge wasiingie na vifaa hivyo kwenye ukumbi wa Bunge.
"Tunaomba sana msije nazo power bank, ni kwenye ukumbi huu simaanishi kwenye eneo la Bunge lote. msiingie nazo power bank wala vifaa vya kuchajia chajia simu hivi ndani ya ukumbi wa Bunge ili kuepuka madhara ya shot (hitilafu) ya umeme na kusababisha moto".
Amesema, baadhi ya vifaa hivyo havina viwango vya maana hivyo vinaweza kusababisha mlupuko na kuhatarisha maisha ya wabunge na wageni bungeni. Spika anatarajia kwamba, wabunge watazingatia agizo hilo na hasa kutoingia na power bank.
Aprili tisa, power bank ya Mbunge ililipuka bungeni na kusababisha moshi na taharuki. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson amelieleza Bunge kuwa, kifaa hicho kililipuka wakati Mbunge anachaji simu mbili.
Aliyasema hayo jana wakati anasoma taarifa ya Spika baada ya kipindi cha maswali na majibu kwenye kikao cha sita cha Mkutano wa 11 wa Bunge la Tanzania.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Tulia, mlipuko huo ulitokea Aprili tisa saa moja 1:20 usiku wakati kikao cha tano kikiendelea.
Mlipuko huo ulisababisha harufu kali, moshi ukatanda katika ukumbi wa Bunge hasa upande wa kulia kwa Spika.
Amesema, kwa mujibu wa maelezo ya askari wa Bunge aliyekuwepo ukumbini, mlipuko huo ulitokea kwenye droo ya Mbunge Richard Mbogo.
|
0 Comments