Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika

WATUMISHI wote wa darasa la saba waliokuwa kazini kabla ya Mei 20, 2004 wakaondolewa kazini, wanatakiwa warudishwe kazini na kulipwa mishahara yao kipindi chote walichokuwa wameondolewa kazini.
Katika utaratibu huo, jumla ya watumishi 7,382 waliosimamishiwa ajira na mishahara yao wakiwemo watendaji wa vijijini 3,817, watendaji wa mitaa 51, watendaji wa kata 253, madereva 330, kada ya afya 1,060 na kada nyingine
1,871 pamoja na watumishi 1,370 waliolegezewa masharti na Katibu Mkuu wa Utumishi. Akitoa Kauli ya Mawaziri bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika alisema wafanyakazi hao waliokuwa kwenye ajira za kudumu, za mikataba au za muda ambao walikuwa kazini kabla ya Mei 20, 2004, warudishwe kazini wote.
Alisema wafanyakazi hao wanaotakiwa kurudishwa kazini ni wale waliokuwa kazini wakati ulipoanza kutumika Waraka wa Utumishi Serikalini Namba 1 wa mwaka 2004. “Warejeshwe kazini mara moja, walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa sheria,” alisema Mkuchika.
Alisema pia watumishi wa umma waliolegezewa masharti ya sifa za muundo kupitia barua ya Katibu Mkuu wa Utumishi ya Juni 30, mwaka 2011, nao warejeshwe kazini mara moja na walipwe mishahara yao kwa kipindi chote, ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira hadi watakapostaafu. Mkuchika alisema uamuzi huo wa kuwarudisha kazini wafanyakazi hao, hautahusu wale ambao waliowasilisha vyeti vya kughushi katika kumbukumbu za ajira zao. Pia, watumishi waliokuwepo katika ajira kabla ya Mei 20, 2004 ambao katika kumbukumbu zao rasmi, kama vile taarifa binafsi katika fomu za tathmini ya utendaji kazi, walijaza taarifa za uongo kwamba wanayo elimu ya Kidato cha Nne na wakashindwa kuthibitisha kwa kuwasilisha vielelezo vya elimu hiyo.
Pia, alisema, watumishi wote walioajiriwa baada ya Mei 20, mwaka 2004, wakiwa hawana sifa ya kufaulu mtihani ya Kidato cha Nne kwa kuwa wajilipatia ajira kinyume cha maelekezo ya serikali. Mkuchika alisema, watendaji na wakuu wa idara za utawala na utumishi wote walioshiriki kuwaajiri watumishi wasiokuwa na sifa ya kufaulu mitihani wa Kidato cha Nne katika utumishi wa umma baada ya Mei 20, 2004, watachukuliwa hatua za kinidhamu. Pia watendaji wakuu na maofisa wote, watakaosimamia mpango huo na wakashiriki katika kuhujumu mkakati wa kuondoa au kuharibu kumbukumbu za watumishi ili haki isitendeke, watachukuliwa hatua za kinidhamu na kijinai.
Alisema uamuzi huo wa serikali, umekuja baada ya kupokea ushauri na maoni kutoka kwa wabunge katika mkutano wa Bunge, unaoendelea pamoja na kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi walioathirika na vyama vya wafanyakazi. Katika Bunge la Bajeti, wakati wa kujadili Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake, wabunge wengi waliomba serikali iwarudishe kazini wafanyakazi wote waliondolewa kazini kutokana na kuajiriwa wakiwa darasa la saba.
Julai 10, mwaka jana, Serikali ilitoa maelekezo kupitia Barua ya Katibu Mkuu wa Utumishi, ikiwataka waajiri kusimamisha mishahara ya watumishi walioajiriwa baada ya Mei 20 mwaka 2004 wakiwa hawana sifa ya kufaulu mtihani wa elimu ya Kidato cha Nne hadi watakapowasilisha vyeti husika. Kwa kutoa uamuzi huo, kunaifanya serikali iwe imetengua uamuzi wa awali wa kuwaondoa kazini wafanyakazi waliokuwa wameajiriwa wakiwa darasa la saba, na kuwarudisha kazini hadi watakapostaafu.