Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeziunganisha Benki za Twiga na TPB na kuwa benki moja kwa malengo ya kuongeza ufanisi wa taasisi za fedha za kiserikali.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo (Jumatano) na Naibu Gavana wa BOT, Bernard Kibesse huku akieleza dhamira ya kuchukua uamuzi huo ni kuleta ufanisi katika taasisi za fedha zilizo chini ya serikali.

Benki hiyo itajulikana kwa jina la TPB Bank hivyo, wateja waliokuwa Benki ya Twiga wataunganishwa na wale wa Benki ya Posta. Mapema mwezi huu, BOT ilitangaza kuwa ipo kwenye mchakato wa kuziunganisha benki hiyo na kuwa benki moja baada ya TPB na Twiga kushindwa kujiendesha. Kutokana na kutetereka kwa benki hizo, mwaka juzi, BOT iliziweka chini ya uangalizi maalum.