Serikali ya Tanzania inajiandaa kukata miti eneo la ukubwa wa asilimia tatu ya hifadhi ya taifa Selous.
Mapema asubuhi ya Jumatano, serikali ilipokea maombi ya zabuni ya kukata miti hiyo kutoka kwa makampuni ya ndani na nje ya nchi yaliyoonyesha nia ya kutekeleza mradi huo wa kukata miti.

Serikali inasema ukataji huu wa miti zaidi ya milioni 2 ni maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme wa megawati 2,100 utakaojengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Hatua hii inaongeza ukosoaji dhidi ya serikali kutoka kwa wanaharakati wa mazingira ambao tangu serikali kutangaza nia ya kujenga mradi huo wa umeme, wamekuwa wakipinga mradi huo kuwa ni hatari kwa wanyama pori na viumbe wengine waishio katika hifadhi hiyo ya Selous, ambayo inatambuliwa pia kama urithi wa dunia.
Rais wa Tanzania Dokta John MagufuliHaki miliki ya pichaIKULU
Image captionRais wa Tanzania Dokta John Magufuli
Wanamazingira watoa tahadhari kuhusu mpango wa serikali
Ni wazi kwamba serikali ya Tanzania imedhamiria kuendelea na mradi huu wa kufua umeme, huku kukiwa na ukosoaji kutoka kwa wanaharakati wa mazingira, ambao wanaelezea wasiwasi wao kuhusiana na athari za hali ya mfumo wa kiikolojia ndani ya hifadhi ya Selous.
Hata hivyo hivi karibuni kuhusu mradi huo Rais John Magufuli aliweka wazi kwamba, serikali yake haitakwamishwa na ukosoaji wa aina yoyote ya kimazingira katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa umeme.
Rais alisistiza kuwa wakati serikali yake inatekeleza sera ya viwanda,mradi huu wa umeme,ni muhimu zaidi kufikia malengo hayo.
Mtendaji mkuu wa wakala wa misitu Tanzania Profesa Dosantos Silayo ameiambia BBC sababu za kuuzwa kwa miti itakayo katwa kwenye hifadhi hiyo kupisha mradi huo.
''Sasa serikali imeona si vizuri kuiondoa miti katika hali ya kuiharibu inaweza kuwa na thamani, serikali imeamua kuitoa kwa utaratibu ambao utaiwezesha iuzwe kwenye makampuni mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza samani ndani na nje ya nchi, hii si biashara, na kwa kweli haijawa nia ya serikali kufanya uharibifu kwenye hifadhi zake''.
Serikali ya Tanzania imesema zoezi la ukataji miti litakuwa salama
Image captionSerikali ya Tanzania imesema zoezi la ukataji miti litakuwa salama
Hata hivyo Mwanasheria wa mazingira Dokta Rugemeleza Nshala amezungumzia ni hatua gani za muhimu kuzingatiwa katika utekelezwaji wa mradi huo.
''Ni kitu ambacho kinapaswa kitekelezwe kwa umakini mkubwa kwa sababu eneo la hifadhi na bado lile eneo wanalotaka kukata miti bado halijatolewa kutoka eneo la hifadhi na ni eneo ambalo ni la urithi la dunia.Umeme unahitajika na mazingira yanahitajika.mazingira yakiharibika hasara ni kubwa zaidi''.
Kikoletwa: Kituo kikongwe cha umeme chageuzwa chuo Tanzania
Kwa sasa Tanzania inayokadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 50,inazalisha kiasi cha megawati 1400 tu za umeme kiwango ambacho hakikidhi mahitaji ya nishati ya umeme ya nchi.
Mradi huu mkubwa wa umeme unatarajiwa kuzalisha kiasi cha megawati zaidi ya 2000 za umeme ili kuimarisha mahitaji halisi ya umeme.