Fatuma Lowassa
UKISEMA unatafuta maisha usisahau kwamba kuna wakati nayo yanakutafuta ili mcheze ngoma moja; tuhuma za Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kudaiwa kutelekeza mtoto zina funzo ndani yake.
Siku chache baada ya msichana aitwaye Fatuma Lowassa kujitokeza ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kutoa madai ya kutelekezwa na Lowassa na hatimaye ishu hiyo ‘kupotelea hewani’, Uwazi limenasa zegwe jipya.

“Kama ni kujitokeza na madai hayo ya kutelekezwa na Lowassa hii si mara ya kwanza kwa msichana huyo, sikumbuki ni lini lakini miaka ya nyuma aliwahi kufanya hivyo.
“Mi nawaamini mkifanya uchunguzi wenu mtapata jambo hili, kuna watu wanayo video ya mahojiano ya msichana huyo pamoja na mama yake wakilalamika kutelekezwa.
“Mimi nimejaribu kuipata nimeshindwa ila nasikia inaandaliwa itolewe ili kufufua upya tuhuma,” chanzo makini kililidokeza Uwazi na kulifanya lipange kikosi kazi kwa lengo la kufuatilia uwepo wa video hiyo.
SIKU TATU ZA UCHUNGUZI
Baada ya kupata taarifa hiyo, Uwazi lilisambaza kikosi kazi chake ambacho kilinusa kila kona ya mitaa ya Jiji la Dar na kuperuzi kidadisi mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo baada ya siku tatu za kazi hiyo mambo yalikuwa wazi.
Ilibainika kwamba baada ya skendo ya waziri huyo mstaafu kuonekana imezimika mara baada ya Fatuma kujitokeza na kuomba radhi familia ya Lowassa kwa kuichafulia jina ndipo ‘wakalia majamvi’ kwa umbea walipoyatandika na kuanza kujadili iweje msichana huyo aibuke kila mara na madai yenye sura moja.
Bila shaka hoja za kwa nini iwe hivyo ndizo zilizoiibua kutoka mafichoni video hiyo yenye tuhuma za Lowassa kumtelekeza Fatuma ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 31, ambayo Uwazi lilidokezwa kuwa ilirekodiwa kitambo kabla mapambano ya Makonda ya kuwasaka waliotelekeza watoto hayajaanza mwanzoni kwa mwezi uliopita.
VIDEO MEZANI KWA UWAZI
Baada ya kazi ngumu ya kusaka nani na wapi video hiyo inapatikana hatimaye Uwazi liliinasa na kubaini kuwa ilirekodiwa kwa mara ya kwanza Juni 16, 2013, eneo la Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar ikiwa na dakika zipatazo 38.
Video hiyo imebeba taswira za mama mzazi wa mtoto anayedaiwa ni wa Lowassa aitwaye Mariam Ally na binti mwenyewe kila mmoja kwa wakati wake wakielezea madai mazito yanayohusu uhalali wa Lowassa kuwa baba wa Fatuma.
Ingawa ipo kiu ya kujua kilichomo ndani ya video hiyo mpya ya mwaka 2013, miaka miwili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ulioiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Mgufuli, busara za Uwazi zimeiweka kando kutokana na watuhumiwa kutopatikana kwa wakati.
Hata hivyo, itoshe kusema kuwa maudhui yake yanafanana kwa kiasi kikubwa na yale ambayo wanalalamika kutelekezwa waliyoyawasilisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda hivi karibuni.
Utofauti unaopatikana kwenye video hiyo ni uwepo wa maneno mazito na ya kushangaza ambayo kimsingi yanafikirisha zaidi kwamba waziri mkuu huyo mstaafu aliyafanya kweli au ndiyo zengwe la kisiasa analodaiwa kufanyiwa na wabaya wake.
KWA NINI ZENGWE JIPYA
Licha ya video iliyonaswa na Uwazi kurekodiwa miaka takribani mitano iliyopita na kuonekana umuhimu wake ulishapita muda mrefu, inaonesha imeibuliwa na wasiojulikana kwa lengo la kuufanya upya mjadala wa uhalali kwa waziri mkuu huyo mstaafu kuwa baba wa Fatuma.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii baadhi ya hoja za wachangiaji zilizokuwa zikibishaniwa ni ile inayohusu mjadala wa madai ya namna ulivyofungwa.
Wengi wamekuwa wakieleza kuwa mpaka sasa haijafahamika wazi ni lipi la kushika kati ya ukweli na uongo juu ya uhusika wa Lowassa katika kadhia hiyo ya kutelekeza mtoto.
Kinachoonekana ni kwamba mara baada ya msichana huyo kujitokeza na kumtuhumu Lowassa kuwa amemtelekeza, siku chache baadaye alijitokeza mbele ya umma na kumuomba radhi Lowassa na familia yake kwa madai ya kumchafua.
Jambo hilo lilimtia matatizoni msichana huyo ambapo alikamatwa na polisi, akahojiwa na baadaye taarifa kutolewa kuwa uchunguzi wake unaendelea na kwamba utakapokamilika atapelekwa mahakamani kwa kosa la udhalilishaji na kusababisha taharuki kwa jamii.
Yawezekana ukurasa wa sakata hilo ndipo ulipoishia maana tangu hapo jeshi la polisi halijatoa na halijaweka wazi nini kinaendelea juu ya msichana huyo na madai yake yanayoibuka kila mara nyakati mambo ya kisiasa yanapokuwa moto.
Kwa mujibu wa ‘sosi’, video ya kwanza ilirekodiwa mwaka 2013, wakati ambao Lowassa alikuwa ni miongoni mwa wagombea urais mwenye nguvu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo hata hivyo alishindwa na Rais Magufuli na kuamua kukihama chama chake na kujiunga na Chadema.
Aidha, mwaka huu nao, kujitokeza kwa msichana huyo miaka miwili kasoro kama ilivyokuwa 2013 kabla ya kuufika uchaguzi mkuu ujao wa 2020 kunatajwa kuwa ni mkakati mchafu wa kisiasa kwa Lowassa.
KAULI ZA LOWASSA
Mara baada ya msichana huyo kujitokeza kwa Makonda na kueleza yake na watuhumiwa wote wa kutelekeza watoto kwa maelfu yao akiwemo Lowassa kutakiwa kufika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar kujibu madai, Lowassa alijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kukana tuhuma hizo.
Hata pale alipotakiwa kwenda kupima vinasaba ‘DNA’, waziri mkuu huyo wa zamani alisema hawezi kufanya hivyo kwa sababu hilo ni jambo la kipuuzi na mara zote alilihusisha na siasa chafu anazofanyiwa.
KUTELEKEZWA KWA FATUMA NI KWA AINA YAKE
Hata kama madai ya Fatuma Lowassa yana ukweli kwamba Lowassa ni mzazi wake, baadhi ya watu wamekuwa wakishangazwa na madai yake ya kutelekezwa kwa sababu ya umri wake wa miaka 31.
“Mimi ukiniambia kutelekeza mtoto halafu ukaniletea mtu kama Fatuma, nitashangaa. Mama mtu mzima anatelekezwaje? Mtu anayeweza kuolewa, kuzaa na kujenga familia yake anakujaje kudai katelekezwa?
“Kwa watoto wa miaka miwili hata 18 siyo mbaya kudai kutelekezwa lakini mtu mzima, unataka kuniambia hata kama angekuwa kwa huyo anayetaka awe baba yake angekuwa amekaa tu anakula bure?” alihoji Aisha Hassan, mkazi wa Mabibo, Dar wakati akizungumza na Uwazi lilipokuwa kazini kupekua habari hii.
KAMERA KWA VIGOGO
Uchunguzi unaonesha kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na vigogo wengi hasa wa nafasi za kisiasa wakituhumiwa aidha kutelekeza watoto, kuzaa nje ya ndoa au kujihusisha bila faragha na wasichana, jambo ambalo kwa maadili ya Kitanzania limekuwa likiwavunjia heshima mbele ya jamii wanayoitumikia.
Kwa msingi huu kamera ya Uwazi hivi sasa iko mitaani nchi nzima ikifuatilia skendo mbalimbali za vigogo na kwamba kila itakayokuwa imeiva itapakuliwa kwenye gazeti bila uoga na kwamba wito wa dawati mbele ya jamii inayopenda ustaarabu ni kutoa ushirikiano wenye lengo la kulinda maadili kwa viongozi wetu.