Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Bw.Antonio Guterres ametangaza uteuzi wa Bi.Joyce Msuya kutoka Tanzania kuwa
naibu katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia program ya mazingira
yenye makao makuu yake Nairobi nchini Kenya.



Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa
mataifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo tarehe 22 Mei, Bi Msuya anachukua
nafasi hiyo kutoka kwa Bw.Ibrahim Thiaw wa Mauritania aliyemaliza muda wake
ambaye katibu Mkuu wa umoja wa mataifa amemuelezea kuwa na utumishi uliotukuka
katika kipindi chake cha uongozi.


Bi.Joyce Msuya amekua akifanya kazi
kama mshauri wa makamu wa rais wa benki ya dunia anayeshughulikia nchi za Asia
Mashariki pamoja na ukanda wa Pasifiki tangu mwaka 2017, makao makuu ya benki
ya Dunia Washington D.C Marekani.


Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Bi.Msuya atatumia muzoefu wake wa miaka 20 katika benki ya Dunia,
pamoja na uzoefu wake katika masuala ya maendeleo ya kimataifa katika kazi yake
mpya na anaimani kuwa ataleta mabadiliko makubwa katika umoja wa mataifa.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo Bi.Msuya
amewahi kufanya kazi kama mwakilishi maalum wa benki ya Dunia na mkuu wa kundi
la benki ya dunia nchini Korea ya kusini,pamoja na mratibu wa taasisi ya benki
ya dunia katika Asia Mashariki na ukanda wa Pasifiki ofisi iliyoko China, na
ameahi kuwa na nafasi mbalimbali za juu katika benki ya dunia na washirika
wake.

Aidha taarifa hiyo imefafanua kuwa
Bi.Joyce Msuya ana Shahada ya uzamili ya Maikrobailojia na kinga kutoka Chuo
Kikuu cha Ottawa, Canada pamoja na shahada ya Baiokemia kutoka Chuo Kikuu cha
Strathclyde,Scotland.



Programu ya umoja wa mataifa ya
mazingira ni mpango wa kidunia wa mazingira unaolenga kutoa mwelekeo katika
uongozi na usimamizi wa mazingira, na kuwashauri wadau na nchi wanachama kwa
ujumla njia sahihi za kutunza na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi
vijavyo. Programu ya umoja wa mataifa ya mazingira inafanya kazi na
serikali,mashirika na asasi za kimataifa duniani kote.