BEI ya vyakula katika nchi za Afrika Mashariki, inatarajiwa kuongezeka katika miezi miwili ijayo kutokana na mavuno kidogo, yatakayopatikana baada ya mazao kuathirika na mafuriko, wadudu na magonjwa.
Kwa mujibu wa Kundi la Usalama wa Chakula, kaya za Rwanda, Uganda, Burundi, Somalia na Sudan, zinazotegemea chakula cha sokoni, zitakabiliwa na upandaji bei kutokana na kupungua kwa bidhaa sokoni.
Ripoti hiyo ni kwa mujibu wa wataalamu kutoka kundi linalofuatilia usalama wa chakula na lishe Afrika Mashariki na Kati (FSNWG). Wiki iliyopita bei ya mahindi ilikuwa Dola za Marekani 402.14 kwa tani huko Kisumu, Kenya na dola 319 huko Ruhuha, Rwanda. Katika mji wa Kabale, Uganda ilikuwa dola 271.02. Wakati miezi sita iliyopita,tani ya mahindi iliuzwa kwa dola 540.28 huko Ruhuha, Uganda 279.38 na dola za Marekani 443.04 huko Nairobi, Kenya, ambapo nchini Burundi, asilimia 60 pekee ya kaya zina chakula.
Hali ya usalama wa chakula inatokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kutokea mafuriko, yaliyosababisha uzalishaji wa chakula kwa baadhi ya sehemu kuharibiwa. Mvua hizo zimesababisha changamoto katika upatikanaji wa masoko ya bidhaa kutokana na ugumu wa matumizi ya barabara, hivyo kufanya vigumu kwa wakulima kusambaza chakula. Mkutano kuhusu usalama wa chakula uliofanyika Nairobi nchini Kenya wiki iliyopita, pia ulitaka wakulima wa Uganda, Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia kuwa makini na kuibuka kwa wadudu waharibifu wa mimea wa viwavijeshi, ambao wamekuwa wkaiharibu mazao machanga. Wadudu hao waligundulika katika wilaya zote 121 wa Uganda, wilaya zote 47 za Kenya na 17 za Burundi na Ethiopia na wilaya zote 30 za Rwanda.
Nchini Kenya wameharibu hekta za mahindi karibu 11,000 na 15,000 na Rwanda zaidi ya hekta 15,300, Ethiopia hekta milioni 1.7 za mahindi zimeharibiwa. Wakulima wametakiwa kujiandaa kukabilia na magonjwa ya mifugo kutokana na hali ya unyevu iliyopo. Nchini Rwanda, Chama cha Wakulima wa Mchele UCORIBU, chenye wakulima zaidi ya 13,000 wanaolima katika wilaya za Gisagara, Huye na Nyanza waliopanda hekta 1,769 za mchele, hekta 612 zimeharibiwa na mafuriko yaliyotokana na mvua. Umoja huo uliokuwa ukikadilia kupata mavuno ya tani 4,826, ambazo ni sawa na wastani wa tani 4.2 kwa kila hekta. Mratibu wa UCORIBU, Jerome Mbonirema alisema mpaka sasa wamekadiria kupoteza asilimia 40 ya mavuno, waliyokuwa wakitarajia katika msimu huu kutokana na mvua.
“Baadhi ya wakulima walichukua fedha katika benki kwa ajili ya kilimo lakini mashamba yao yameharibiwa na mvua, hivyo tunaziomba benki kusaidia kubadilisha utaratibu ili wakulima waweze kulipa kwa msimu ujao ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia riba, ikiwa ni pamoja na serikali kutafuta namna ya kuwasaidia wakulima ili waweze kulima tena,” alisema. Wizara ya Usimamizi wa Majanga na Wakimbizi (MIDIMAR), imesema kutoka Januari mpaka Mei 10 mwaka huu, takwimu zinaonesha hekta 4,973.5 zimeharibiwa na mvua.
Serikali ya Rwanza imeunda timu kwa ajili ya kuwahamisha raia, wanaoishi katika maeneo hatarishi kutokana na athari za mvua zinazoendelea. Timu hiyo imeundwa na watu kutoka wizara mbalimbali ikiwemo MIDIMAR, maendeleo ya jamii, miundombinu, mazingira, afya, kilimo na mifugo na ulinzi. Waziri Mkuu, Edouard Ngirente akitangaza timu hiyo, alizihakikishia familia zilizoathirika na mvua kuwa serikali iko pamoja nao na itawapa misaada ya dharura na ya muda mrefu. Waziri Mkuu na mawaziri wengine, wiki hii wamefanya ziara katika maeneo ya Karongi, Rutsiro, Rubavu, Ngororero, Nyabihu, Gakenke na Burera, ambazo ni wilaya zilizoathirika na mvua hizo na kuhitaji msaada wa serikali. Familia 853 kwa miezi minne zimehamishwa katika makazi yao, huku mwanzo wa mwaka serikali imetoa mashuka yenye thamani ya faranga milioni 141, zaidi ya faranga milioni 200 kujenga vyoo salama na fedha za dharura kusaidia familia zilizoathirika.