Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akihutubia mamia ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni. Picha Zote Na Mathias Canal, Wazo Huru blog
Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakifatilia hotuba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni.

Na Mathias Canal, Bukombe-Geita

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri
wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alilolitoa 2 Aprili 2018 wakati
wa dhifa ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika
uwanja wa Magogo mkoani Geita Katika sherehe hizo zilizonakshiwa
na Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ambayo ni ‘Elimu ni ufunguo
wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’

Waziri
Mkuu aliwagiza viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo
inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za msingi na kwa sekondari
wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio
 endelevu shuleni kwani miongoni mwa sababu zinazopelekea
wanafunzi kutoelimika ipasavyo ni pamoja na utoro shuleni.

Kupitia agizo hilo Mhe
Biteko
amechangia mabati 100
geji 28 yenye thamani ya Sh 2.6 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa kupaua vyumba
vya madarasa katika shule ya sekondari Azimio Wilayani Bukombe ikiwa ni sehemu
ya hamasa kwa wanafunzi kuwa na maeneo bora ya kusomea.



Mara baada ya uzinduzi wa Mwenge huo wa Uhuru 2 Aprili 2018 kabla
ya kuelekea Mjini Dodoma kwa ajili ya shughuli za Bunge zilizoanza 3 Aprili
2018 Mhe Doto Biteko alizuru Kijiji cha Nampalahala kilichopo Kata ya Busonzo
na kujionea jinsi ujenzi wa maabara unavyoendelea ambapo pia alichangia matofali 10,000  kwa ajili ya ukamilishaji Wa vyumba vya
maabara ili kurahisisha uanzishaji wa shule ya sekondari wa Kata ya Busonzo wilayani
Bukombe
.


Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa, Mhe
Biteko alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli, imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu
ya Awali hadi Elimu ya Juu hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa maendeleo
ya wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu bure
kwa wanafunzi wote nchini kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari hivyo jukumu
la wazazi ni kuwapeleka watoto shule ili kunufaika na matunda ya serikali
katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaja 2015-2020.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kukiunga mkono Chama Cha
Mapinduzi kwani ndicho chama pekee nchini kinachoshughulika na matatizo ya
wananchi ikiwemo kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo katika kuboresha
elimu, afya, miundombinu na huduma zingine zikiwemo upatikanaji wa maji.