Kiongozi wa Kikundi cha akinamama cha Kitanga Green Voices, Mama Abia Magembe, akitoa maelezo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo kwa wageni mbalimbali, akiwemo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella.


NA DANIEL MBEGA, KISARAWE
KUWEKWA kwa jiwe
la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika Kijiji cha
Kitanga wilayani Kisarawe kumetoa fursa kubwa kwa kikundi cha akinamama
wanaojihusisha na kilimo cha zao hilo pamoja na wananchi wengine.
Kiongozi wa
Kikundi cha akinamama cha Kitanga Green Voices, Mama Abia Magembe, anasema
uwekaji wa jiwe hilo la msingi uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe
Jumamosi, Septemba 15, 2018 umefufua matumaini si ya akinamama pekee, bali hata
wananchi wengine ambao walikuwa wamekata tamaa ya kulima muhogo kutokana na
kutokuwepo kwa soko la uhakika.


“Matumaini sasa
yapo ingawa bado tunayo safari ndefu ya kufikia malengo, tunataka kuchakata na
hatimaye kutengeneza bidhaa mbalimbali zaidi ya 300 kwa kutumia zao la muhogo,” anasema Mama
Magembe, Ofisa Kilimo mstaafu ambaye amefufua upya matumaini ya wakulima wa eneo hilo.
Tayari amekwishawafundisha akinamama zaidi ya 60 kijijini hapo ambao wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo na anaendelea kuwafundisha wengine, kwani anasema, mahali kilipo kiwanda hicho patakuwa kituo cha kudumu cha mafunzo kwa wote, wanaume kwa wanawake.
Wakati wa uzinduzi
huo, DC Mwegelo aliahidi kuwasaidia akinamama hao pamoja na wakulima wengine
kukuza zao la muhogo, ambalo alisema ni miongoni mwa mazao mawili ya kipaumbele
wilayani humo, likiwemo zao la korosho.
Alisema
atawasaidia akinamama hao kuwaunganisha na wadau mbalimbali ili kupata mikopo
nafuu, ikiwemo mikopo isiyo na riba huku pia akiahidi kwamba, changamoto ya
umeme na maji zitatatuliwa haraka.
Pengine unafahamu
faida tatu au nne tu za muhogo ambazo ni kuutafuna mbichi, kuuchemsha au
kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na
dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama kuni.
Inawezekana hujui
kama maganda ya mihogo baada ya kumenywa ni chakula bora cha mifugo yakikaushwa
au mabichi.
Siyo ajabu pia
hujui kwamba muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yake yanatoa wanga
(starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi
za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.
Lakini zao la
muhogo ni zaidi ya linavyofikiriwa kwa sababu licha ya faida hizo chache,
lakini pia linazalisha bidhaa zaidi ya 300 kama ambavyo akinamama wa Kijiji cha
Kitanga, Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe wameamua kufanya.
Akinamama hao
kupitia kikundi chao cha Kitanga Green Voices mbali ya kuzalisha unga pamoja na
chips, sasa wanatengeneza bidhaa lukuki zenye ubora kama chapatti, maandazi,
skonzi, biskuti, tambi, cassava chop, na nyinginezo nyingi.
Hatua hiyo imekuja
baada ya kupatiwa mafunzo kupitia mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na
taasisi ya maendeleo ya wanawake wa Afrika inayojulikana kama Women of Africa Foundation,
ambayo iko chini ya Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania,
María Teresa Fernández de la
Vega.
Kuanzishwa
kwa mradi huo wa kusindika muhogo pamoja na bidhaa zake kumeliokoa zao hilo
ambalo licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, lakini limekuwa likidorora
hata katika soko la vyakula.
“Tangu tumeanzisha
kikundi hiki miezi mitatu iliyopita hivi sasa muhogo hauwezi kuozea shambani na
wananchi wanaona umuhimu wa zao hilo,” anasema Mama Magembe, ambaye ni mratibu
wa mradi huo.
Mama Magembe, ambaye yeyé
pamoja na akinamama wengine tisa walipatiwa mafunzo nchini Hispania kwa nia ya
kuanzisha shughuli za ujasiriamali unaoendana na utunzaji wa mazingira pamoja
na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, anasema kwamba zao la muhogo sasa
limepata thamani kubwa kijijini hapo na wana uhakika wakulima wa wilaya ya
Kisarawe wanaweza kugeukia miradi kama hiyo ili kuongeza mnyororo wa thamani.
Akinamama 10 wanaofanya
miradi mbalimbali ya ujasirimali kutpia mradi wa Green Voices wanatoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma,
Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Silvera Mujuni,
Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, anasema kwamba wilaya hiyo ina
fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi yatokanayo na muhogo kwa kuwa
zao hilo ndilo kuu kwa chakula na biashara.
Anasema kwamba,
ardhi katika vijijini vingi vya wilaya hiyo inastawisha muhogo kwa wingi, hivyo
ikiwa wananchi watajizatiti na kujifunza namna ya kuchakata bidhaa za muhogo
wanaweza kupata faida kubwa kiuchumi.
“Muhogo ndilo zao
kuu katika maeneo mengi ya wilaya hii ambayo haiwezi kustawisha mazao mengine
kama mahindi, hivyo ni vyema wananchi wakajifunza utengenezaji wa bidhaa
mbalimbali zinazotokana na zao hilo,” anasema Bi. Silvera aliyemwakilisha
mkurugenzi wa wilaya hiyo na ambaye ndiye alikuwa akiwafundisha akinamama hao
namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Awali Ofisa
Mtendaji wa Kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, aliwataka akinamama hao wajipange
wasajiliwe rasmi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na
taasisi nyingine za binafsi.
“Ofisi yangu iko
wazi wakati wote, mkitaka kwenda kusajiliwa wilayani hata leo niko tayari
kuwasaidia, nawaombeni mje niwasaidie hata namna ya kuandaa katiba ya kikundi
pamoja na taratibu nyingine,” alisema.
Naye Diwani wa
Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, amesema atajitahidi – kwa kushirikiana na diwani
mwenzake wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya – kuwapigania akinamama hao
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kupatiwa misaada na mikopo hata
kupitia katika asilimia 10 ya bajeti ya halmashauri ambayo hulenga kuwasaidia
wanawake na vijana.
“Bahati nzuri sisi
hapa ni madiwani wanawake, kwa hiyo tutalipeleka suala la akinamama hawa kwenye
Baraza la Madiwani na kuelezea umuhimu wa kuongeza thamani kwenye zao letu la
muhogo ili limkomboe mkulima,” alisema Diwani Lilomo.
Mratibu wa Mradi
wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, anasema kwamba
anafarijika anapoona wanawake wakihamasika kushiriki shughuli za maendeleo,
hasa ujasiriamali unaolenga kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Suala la
kuhakikisha usalama wa chakula, kutokomeza umaskini, kuwawezesha wanawake
kiuchumi na mapambano dhidi ya tabianchi ni mambo yaliyopewa kipaumbele katika
Malengo Endelevu ya Dunia, hivyo wanawake wanaotekeleza miradi ya Green Voices
wanayatekeleza malengo hayo kwa wakati mmoja,” anasema Secelela.

Zao lililotelekezwa, sasa mkombozi
Muhogo ni zao
linalochukuliwa na wengi kama la ziada hasa kwenye ukame, lakini wengi
hulifanya kama mlo wa hamu bila kutambua kwamba zao hilo lina manufaa makubwa kwa
lishe na kibiashara.
Wengi
wanauchukulia muhogo kama chakula cha maskini, hawa wale wanaojitiahidi kulima
zao hilo, huyapa kipaumbele mazao mengine kuliko muhogo.
Lakini muhogo ni
zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha jamii na baa la njaa huku katika baadhi
ya mataifa likitumika kama chanzo cha nishati ili kukabiliana na bei ya mafuta
na nishati nyinginezo.
Baa la njaa ni
tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi barani Afrika, Tanzania ikiwa miongoni
mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima muhogo, bado wanalipuuza zao hilo
na kuliona kama zao fulani la mizizi tu.
Katika mikoa kama
Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi inalima kwa wingi muhogo, chakula chao
kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.
Licha ya
kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta mlo wa siku hiyo umetokana
na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana kuni zilizopikia ni matawi
ya muhogo, ugali wa muhogo na kisamvu cha muhogo!
Na wakulima wengi
katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara wanakula ugali wa muhogo pale wanapokoa
unga wa mahindi, ambapo wanaokula ugali huo wa muhogo (Wazaramo wanasema ‘bada’
na Wamakua wanauita ‘matamba’) huonekana maskini wa kutupa.
Leo hii
wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya kustahimili ukame, bado wengi
wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa muhogo unatoa bidhaa nyingi
zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao hilo na kulima kibiashara.
Inafurahisha sana
siku hizi kuona watu wengi wakikimbilia ugali wa muhogo hata hotelini, lakini
hiyo bado haijatosha kulirasimisha zao hilo ili liwe na tija kubwa.
Akinamama wa
Kijiji cha Kitanga wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa zao hilo, kwa sababu tayari
wameanza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo hata wananchi wa kijiji hicho
wameshangazwa nazo baada ya kuzionja na kuona ubora wake.
Kilimo cha muhogo
siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira
pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za Marekani 20 milioni sawa na
Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula nje, jukumu ambalo kikundi cha
Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.
Faida za muhogo ni
nyingine kama zilivyoelezwa hapo juu, lakini kwa msisitizo ni kwamba, unga wake
hutumika kutengeneza vyakula mbalimbali, baadhi ni uji na ugali, vitafunwa kama
keki, mikate, skonzi, biskuiti, mandazi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, kuni,
mboga, huksi pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Mazao
yanayopatikana katika mzizi wenyewe, miti na majani huweza kuzalisha bidhaa
anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta, kilevi, dawa za
binadamu na plastiki wakati ambapo wanga (starch) hutumika kutengeneza dawa za
madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup).
Takwimu za kilimo
cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa
kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani milioni 102.6 kila
mwaka.
Tanzania ni nchi
ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya
Nigeria,
Ghana na Kongo DRC

ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika
kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi
nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa
inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga,
Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni
wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma
huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania. 
Muhogo
ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya
mahindi.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya
Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi
kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na
magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi
katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga
mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na
kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.