Maryann Mungai
Image captionMaryann Mungai - anatumia fursa hii kuwasihi watu ambao wana ulemavu wa ngozi kama yeye kujitokeza
Wanamitindo wenye ulemavu wa ngozi wameshiriki katika shindano la kuiwakilisha Kenya katika mashindano makubwa ya Afrika mashariki ya kumtafuta bibi na bwana Albino.
Jamii ya albino imekumbwa na unyanyapaa na hata wengi kuyapoteza maisha yao kwa watu wanaoamini kwamba sehemu za mwili za watu wenye ulemavu wa ngozi yaani albino zinaweza kuwapatia utajiri.

Watu hao wamekuwa wakibaguliwa na hata kuitwa majina yasiostahili.
Mashindano haya yamenuiliwa ubadili mtazamo wa jamii dhidi ya walemavu hawa. Miongoni mwa walioshiriki ni pamoja na:
Maryann Mungai (wa pili kushoto) miongoni mwa kundi la wanamitindo wenye ulemavu wa ngozi
Image captionMaryann Mungai (wa pili kushoto) miongoni mwa kundi la wanamitindo wenye ulemavu wa ngozi
Maryann Mungai - Nakuru Kenya
Ninafuraha kwa kuchaguliwa kuliwakilisha taifa langu, licha ya kwamba kuna wakati watu huniita majina yasiofurahisha kama vile mzungu, pesa na zeruzeru.
Kushiriki kwangu katika shindano hili nikuwasihi watu ambao wana ulemavu wa ngozi kama mimi kujitokeza.
Iwapo nitakuwa mshindi nitaenda mashinani kuwatafuta watu wenye ualbino na hata watoto wengine wapate elimu.
Clinton, Oytita
Image captionClinton Oytita - 'Ualbino sio kitu kibaya bali ni kitu cha kujivunia, sisi ni wanadamu kama nyinyi'
Clinton, Oytita- Kisii Kenya
Nashukuru jinsi nilivyoumbwa kwani hakuna kitu ninachoweza kukibadili katika maisha yangu na iwapo nitashinda taji hili la Afrika mashariki basi nitawafahamisha wote wasiojua kuhusu ualibino.
'Ualbino sio kitu kibaya bali ni kitu cha kujivunia, sisi ni wanadamu kama nyinyi'. Kwa hivi sasa matusi yamepungua na ningependa yaishe kabisa hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Valencia Bosibori - Mombasa Kenya
Awali ilikuwa vigumu kutembea barabarani, lakini wakati huu unaweza kutembea na mtu akakuita akasema wapendeza! Hilo ni jambo kubwa sana.
Wazazi wangu walikuwa na wakati mgumu kuielewesha jamii wakati nilipozaliwa.
Nilipelekwa shule maalum na baadaye nikajiunga na shule ya watu wa kawaida na shule hiyo ilinisaidia kufahamu mambo mengi zaidi.
Valencia Bosibori
Image captionValencia Bosibori
Oree Wakhulonga -Eldoret Kenya
Watu wenye ualbino bado hawaheshimiki lakini kupitia kwa nyimbo zangu natumai heshima kwa watu wenye ulemavu wa ngozi wataweza kuheshimika.
Wakati wakumtafuta mchumba kweli hapo huwa ni changamoto kubwa kwani kuna watu ambao hawana uelewa kuhusu hali ya ualbino kwa hivyo talata yangu na kisomo changu ndicho ninachokitengemea.
Natumaini kumuoa msichana mrembo wa kawaida mwenye melanin asilimia 66.
Tamasha hilo iliandaliwa na shirika la kitaifa la watu wenye Ualbino Kenya ( ASK) kwa lengo la kuwapatia nafasi katika jamii.
Kulingana na Mwenyekiti na mshirikishi wa kitaifa wa watu wenye ualibino Kenya au ASK, Isaac Mwaura, watu wenye ualibino hawana haki, nafasi katika jamii , hutengwa , hudharauliwa na hawapatiwi hadhi kama watu wengine.
Mwaura amesema lengo kuu ni kutafuta mwafaka kwa watu wenye ualbino wawe wanajihisi kama binadamu wengine kukubalika na kupatiwa jukwaa la kuonyesha talanta zao.
Isaac Mwaura - Seneta mteule Kenya
Image captionIsaac Mwaura - Seneta mteule Kenya (Alivaa nguo ya njano) anasema nimuhimu kwa watu wenye ualbino kupatiwa jukwaa la kuonyesha talanta zao
''Nilipokuwa mdogo nilikuwa na ndoto ya kuwa mbunge lakini wazazi wangu hawakuamini hilo.
Nafurahi kwamba mimi ni Seneta maalum mwenye ualibino na natumai watu wengi wataniiga na hata tuwe na rais mmoja wa Afrika mwenye Ualibino kama sio Kenya.
Wakati nikigombea ubunge watu hawakutaka kunisalimia kwa mkono au mtu anakusalimu na baadaye anapangusa mkono wake akiwa na anafikiria kwamba nitamuambukiza''.
''Katika mapenzi pia watu walikuwa wakisema nitapata mtoto wa namna gani lakini nimeona na hata nina watoto watatu lakini wawili walifariki''.
Isaac amewasihi wazazi wanaowapata watoto wenye Ualibino, wasiwatoroke watoto wao hasa wanaume. Ameeleza kwamba ni jukumu la mzazi kuwasaidia watoto na kulea vipaji vyao ambavyo vitawasaidia katika siku za usoni.
Shindano hilo la kumtafuta bibi na bwana ualbino litaandaliwa tarehe 30 Novemba nchini Kenya ambapo wanamitindo 30 kutoka taifa la Kenya, Uganda na Tanzania watashiriki.
Mpiga picha: Peter Njoroge